Mkuu wa Mkoa
wa Kigoma, Emmanuel Maganga ameongoza mamia ya wananchi mkoani hapa katika
mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Mjini, Amani Kabourou
aliyefariki dunia Machi 7, 2018 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili
(MHN) alipokuwa akipatiwa matibabu.
Kabourou
amewahi kuwa mbunge wa Kigoma Mjini mwaka 1995-1999 na 2000-2005 kupitia
Chadema, mwaka 2006 alijiunga CCM na kuchaguliwa mbunge wa Bunge la Afrika
Mashariki. Mwaka 2012 hadi 2017 alikuwa mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kigoma.
Akitoa salamu
za rambirambi leo Machi 9, 2018, Maganga amesema Kabourou alikuwa mwana mageuzi
na ndiyo maana alikubalika na kupata uongozi katika nyanja mbalimbali ndani na
nje ya nchi
Amesema ni
vyema wananchi wa Kigoma na Taifa kuiga mema yaliyofanywa na marehemu katika
jamii ikiwa ni pamoja na kutoa ushirikiano kwa kila mtu bila kujali umri,
itikadi au chama chake.
Akimzungumzia
Kabourou, Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe amesema
marehemu ana historia kubwa na ya pekee katika mkoa huo kwani ndiye
aliyewafungua macho kisiasa.
Amesema mkoa
huo uliokuwa nyuma kisiasa kabla ya Kabourou kuingia kwenye siasa na baada ya
kuingia watu wengi walipata mwamko na kuanza kujua haki zao na kuzisemea
"Sisi
wengine hapa mnavyotuona ni matunda ya kazi ya Dk Kabourou. Pamoja siku za
nyuma tulitofautiana lakini aliendelea kuweka masilahi ya wana Kigoma
mbele," Amesema Zitto.
Pia, mbunge
huyo amesema tayari ameiagiza Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma ujiji
kuitisha kikao maalumu kupitisha jina la Dk Kabourou ili liwe jina la
barabara ya kutoka na kuingia kiwanja cha ndege cha Kigoma.
Mwenyekiti wa
CCM Kigoma, Ammandus Nzamba amesema Dk Kabourou enzi ya uhai wake
alikuwa mtu wa kusimamia anachokiamini na kutoyumbishwa na kitu chochote.
Katibu mwenezi
wa Chadema Wilaya ya Kigoma Mjini, Idd Ngesha amesema kifo cha mwanasiasa huyo
kimeacha pengo kubwa kwani alikuwa na mchango katika kukipaisha chama hicho.
Dk Kabourou
aliyekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa mapafu, ameacha mke na watoto 12.
Rc Maganga aongoza Mamia kumzika Dk Kabourou
Reviewed by KUSAGANEWS
on
March 09, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment