"Fumbua Kinywa chako kwa ajili yake aliye
bubu; Uwatetee watu wote walioachwa peke
yao; Fumbua kinywa chako, uhukumu kwa haki; uwapatie maskini na wahitaji haki yao" (Mithali
31: 8-9)
Tunapoadhimisha sikukuu ya kukumbuka
kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo,tunatambua kuwa utume wa Kanisa letu katika
taifa letu, unafanyika katikati ya changamoto kadhaa. Kwa kuwa Kanisa ni sehemu
ya jamii, linaguswa na changamoto hizo.
Katika kukaa pamoja na kuliombea taifa letu,
sisi maaskofu wa KKKT, tumetafakari na kubaini changamoto hizo. Kwa njia ya
salaam za Pasaka,
tunaleta kwenu changamoto tatu ili ziongeze
mzigo wa kuliombea taifa letu na viongozi wake.
1. Jamii na Uchumi:
Kiini cha Utume wetu katika jamii
kinatuingiza kwa nia njema katika maisha ya uchumi na mshikamano wa kijamii.
Neno la Mungu linatufundisha kuwa "Mwanadamu hawezi kuishi kwa mkate peke
yake" (Luka 4:4).
Pia neno la Mungu linatuhakikishia kuwa
Bwana wetu Yesu Kristo alikuja ili tuwe na uzima tele (Yohana 10:10). Tunawiwa
katika umoja wetu wa ubaba, kuipongeza Serikali yetu kwa jitihada inazofanya
kuboresha maisha ya wananchi.
Tumeshuhudia jitihada na nia njema kuhusu
uvunaji na umilikaji wa raslimali za
nchi kwa manufaa ya taifa zima. Aidha, tunapongeza jitihada za
ukusanyaji wa kodi ili kuiwezesha Serikali
kugharamia huduma za jamii.
Hata hivyo, bila kukatisha tamaa jitihada
hizo, tunawiwa kushauri yafuatayo:
I. Sekta binafsi na mashirika ya dini ni
wadau wa maendeleo, si washindani wa
serikali katika kuchangia maendeleo ya taifa. Mazingira yasiyo rafiki
kuhusu wadau hawa, ni kikwazo kisicholeta
mshikamano kati ya serikali na sekta binafsi na mashirika ya dini katika kuleta
maendeleo. Jitihada za
makusudi na za mara kwa mara zifanyike
kuondoa dhana ya ushindani
kati ya serikali na wadau hawa ili
kuimarisha mahusiano mema kati ya serikali na sekta binafsi.
II. Ili mfumo wa ukusanyaji wa kodi uwe
endelevu; jitihada za kukusanya kodi ziendane na elimu kwa mlipa kodi.
Msisitizo wa uzalendo wa kulipa kodi uende sambamba na ustawi wa walipa kodi
katika shughuli zao za biashara.
Mivutano isiyo na tija kati ya walipa kodi
(wafanya biashara) na mamlaka ya ukusanyaji wa kodi, inastawisha uadui
unaopunguza makusanyo ya kodi na kujenga ushawishi wa rushwa. Mfumo wa kodi unaowafilisi
wafanya biashara, haulengi kujenga uchumi wa viwanda.
III. Kutokana na ongezeko kubwa la vijana
wasio na ajira; jitihada za wazi na za makusudi zifanyike ili msukumo wa uchumi
wa viwanda ufikie matumaini yanayoshikika miongoni mwa vijana wasio na ajira.
Sekta binafsi, wawekezaji na wadau wengine, wahakikishiwe usalama wa mitajiyao
kisheria. Hili likifanyika ni kichocheo kizuri cha ujenzi wa viwanda.
IV. Uchumi wa viwanda (vidogo na vikubwa)
uendane na uwekezaji katika sekta ya kilimo maeneo ya vijijini. Kilimo na
ufugaji ndizo sekta zenye wigo mpana wa
viwanda vinavyogusa maisha ya watanzania walio wengi.
Utozaji holela wa kodi na ushuru wa mazao
unakatisha tamaa wadau wa kilimo. Migogoro kati ya wakulima na wafugaji kwa
upande mmoja, na wakulima/wafugaji na wawekezaji kwa upande wa pili, si kivutio
cha uwekezaji katika sekta ya kilimo.
2. Maisha ya Siasa:
Kwa umoja wetu katika utume, tunatambua
siasa safi na uongozi bora kuwa ni misingi iliyoongoza maisha ya siasa katika
taifa letu. Ujio wa vyama vingi mnamo 1992, haukuondoa umuhimu wa misingi hii bali
ulipanua matumizi ya demokrasia iliyojengwa katika uhuru wa mawazo.
Taifa ni mkusanyiko wa taasisi na watu
mbalimbali, wenye lengo moja lakini kwa njia mbalimbali. Kutokana na wingi huu,
taifa letu daima ni juu ya vyama, taasisi na makundi.
Taifa huongozwa na katiba iliyo kiini cha
sheria zote. Taifa haliongozwi na Ilani za vyama. Serikali haiongozwi na Ilani
za vyama. Serikali huongozwa na Katiba, Sheria, kanuni na mapokeo mema (misingi
na tunu za taifa).
Serikali husimamiwa na Bunge huru lililo sauti
ya wananchi. Wananchi ndilo chimbuko la madaraka ya Bunge. Bunge halisimamiwi
na ilani, chama chochote wala mtu awaye yote. Kwa umoja wetu na kwa nyakati
zetu, hivi sasa tunashuhudia matukio yaliyo kinyume na tunu na misingi
iliyolilea taifa letu.
Baadhi ya matukio hayo ni:
I. Hofu iliyojengwa katika matukio halisi
yakiwamo utekaji, utesaji, kupotea kwa watu, mashambulizi ya silaha dhidi ya
viongozi wa kisiasa, mauaji yenye mwelekeo wa kiitikadi, vitisho, ubambikiziaji
wa kesi, na matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya wananchi.
II. Kupungua na hatimaye kutoweka kwa uhuru
wa kujieleza, kukusanyika, na kupata habari. Kwa mwenendo huu, kuna hofu kuwa
hata uhuru wa kuabudu uko mashakani.
III. Kubanwa na hatimaye kuelekea kupungua
kwa uhuru wa Bunge, Mahakama, na Tume ya Uchaguzi. Hatua hii ni pamoja na
kudhoofishwa kwa serikali za Mitaa.
IV. Kukosekana kwa mazingira ya haki na
uhuru wa kuchagua na kuchaguliwa katika chaguzi mbalimbali. Chaguzi zote
zimeghubikwa na ubabe, vurugu, hila, na vitisho.
V. Utekelezaji wa mipango ya maendeleo wenye
mwelekeo wa kiitikadi. Hatua hii imeimarisha ubaguzi wa kiitikadi katika taifa
letu na kukuza migawanyiko.
VI. Kushamiri kwa chuki mioyoni mwa watu
ambalo ni chimbuko la visasi, kukata tamaa, na ushiriki mdogo wa wananchi
katika chaguzi na maisha ya siasa.
VII. Udhalilishaji wa kauli njema isemayo
"Maendeleo hayana chama". Udhalilishaji huu unafanyika kwa njia ya
kutumia fedha nyingi katika chaguzi ndogo zinazotokana na watu wanaobadili vyama
ili kuleta maendeleo. Tunajiuliza, kama maendeleo hayana chama, kwa nini mtu
anajiuzuru chama fulani, eti kwenda kuleta
maendeleo katika chama kingine? Mchezo huu unagharimu fedha nyingi na maisha ya
watu wanaokufa, kujeruhiwa na uharibifu wa mali.
Mambo haya ni tishio linalohatarisha umoja
na amani ya nchi yetu.
3. Masuala Mtambuka
Kanisa ni alama ya uwepo wa utume wa kuleta
na kutunza matumaini katika jamii. Ukimya wa Kanisa katika masuala yanayoigusa
jamii ni ukwepaji wa wajibu wake.
Lakini pia sauti ya Kanisa isiyomilikiwa na
mtu isipokuwa Mungu tu, ni chachu ya amani na matumaini. Kwa dhamiri safi inayotokana
na utambuzi wa "Wakati wa Mungu"(Kairos) katika taifa letu, tunawiwa kutambua
masuala mtambuka yanayogusa maisha ya watu kipekee na kwa njia nyingi na
kuyatolea ushauri ufuatao:
I. Kuhitimisha mabadiliko ya mara kwa mara
katika mfumo wa elimu nchini ili kuondoa mwanya wa kila mtendaji mkuu wa
wizara kuja na sera yake.
Elimu ni kitovu cha ustawi wa taifa, kisiwe
kinachokonolewa
chokonolewa kila wakati. Sekta zote nchini
hujenga mafanikio yake katika mafanikio ya mfumo thabiti wa elimu.
II. Uwezeshaji wa vijana kupata mikopo ya
elimu ya juu uwe shirikishi na usiokuwa na "ubaguzi" kati ya
wanafunzi wa vyuo binafsi na wale wa serikali; sayansi na sanaa; wazazi maskini
na wenye nafasi; waliosoma shule binafsi na wale wa shule za serikali, n.k. Kwa
kuwa huu ni mkopo, jitihada ziwekwe zaidi katika urejeshaji wa mkopo huo kwa
kuzingatia kuwa huu ni mkopo kwa mtoto
siyo kwa mzazi.
III. Vyombo vya usimamizi wa sheria na
utoaji haki vionekane vinatenda haki sawa kwa watu wote na makundi yote bila
kuacha ishara za fadhila au kukomoana.
IV. Wajibu wa serikali kikatiba katika
kulinda uhai wa raia wake, uonekane unatekelezwa bila kuacha mwanya wa
kuituhumu serikali. Ukiachwa mwanya katika ulinzi wa uhai wa raia, waweza
kutumiwa na mamluki kujichukulia sheria mkononi kwa niaba ya serikali. Damu
isiyo na hatia
ina madhara kwa kizazi hiki na vizazi
vijavyo. Mpaka sasa tumeshuhudia umwagaji wa damu unaotusuta sisi sote na
mamlaka zote. Mungu anatusuta watanzania kama alivyomsuta Kaini: "Sauti ya
damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi" (Mwanzo 4:10).
V. Uhai wa mtu una thamani isiyopimika. Ni
wajibu usiokwepeka kuulinda na kuutunza uhai kwa vitendo halisi. Endapo uhai
umepotea katika mazingira yoyote, uchunguzi huru na wa haki ufanyike na taarifa
zitolewe kwa wakati muafaka ili kujenga jamii yenye imani kwa serikali na vyombo
vyake. Matukio ya mauaji ya askari wetu, mauaji ya raia, majaribio ya kuwaua
wanasiasa, utekaji, na uteswaji visipochunguzwa na kutolewa taarifa, ni shina la hofu na
uchungu katika jamii. Jamii iliyojaahofu na uchungu, haiwezi kuwa na maendeleo
wala kuwa na roho ya uzalendo.
VI. Ili kulipatia taifa letu ufumbuzi wa
mambo yote tuliyotaja na kushauri kwa wakati huu na ujao; tunaisihi serikali ya
awamu ya tano, kurejea
mchakato wa upatikanaji wa KATIBA MPYA ya
wananchi,
iliyopendekezwa na wananchi kupitia Tume ya
Warioba. Watanzania wengi wanaona na kuamini kuwa KATIBA MPYA ina majibu ya
kukidhi mahitaji ya taifa letu kwa sasa na baadaye. KATIBA MPYA ni zao la
utashi wa Watanzania kupitia tume ya Warioba iliyokuwa na uwakilishi mpana wa
taifa letu.
VII. Aidha, tunawashauri raia wema, kwa njia
za kidemokrasia kupitia majukwaa ya kikatiba yaliyo katika maeneo yao, kudai
upatikanaji wa KATIBA MPYA. Itapendeza ikiwa KATIBA MPYA itapatikana kabla ya uchaguzi mkuu ujao.
Mambo mazuri
yanayofanywa na serikali ya awamu
ya tano yatadumu iwapo kuna KATIBA MPYA
inayolinda mazuri.
Kiongozi mzalendo si mbadala wa KATIBA MPYA.
Tanzania yenye amani na maendeleo ni tunda la itikadi zote, dini zote, makabila
yote na makundi yote chini ya KATIBA MPYA.
C. HITIMISHO
Kufufuka kwa Yesu Kristo ni kiini cha
Matengenezo ya Kanisa. Kwamba, katikati ya jamii iliyokata tamaa na kutawaliwa
na hofu, Kristo alifufuka na kuleta matumainimapya. Kwamba, katikati ya
wasiwasi wa Kanisa kupoteza nguvu ya utume wake, Roho Mtakatifu aliongoza
Matengenezo ya Kanisa.
Kwa hiyo Matengenezo ni endelevu katika
jamii ya watu na taasisi zao. Muasisi wa Matengenezo Dr. Martin Luther yungali
analiwajibisha Kanisa kuzingatia utume wake unaoleta matumainimapya kila siku.
Waliobatizwa wote ni wamisionari tunaotumwa
na Bwana wetu Yesu Kristo (Yohana 20:21). Imetupasa kuwa nuru na chumvi ya
jamii na kuwa mawakala wa uhuru, umoja na amani.
Taifa letu lilipata uhuru mwaka 1961 bila
kumwaga damu. Roho ile ile ya
majadiliano na maridhiano iliyokuwamo ndani
ya waasisi wa taifa letu, inatakiwa
kila wakati. Uhuru ulioletwa kwa
majadiliano, utunzwe na kulindwa bila ulazima wa kumwaga damu ya watanzania.
Uhuru na Umoja ndizo ngao zetu zilizolitunza taifa kwa zaidi ya miaka 50.
Sisi tulio maaskofu kwa neema ya Mungu,
tunaleta wito kwenu wenye imani katika dini mbalimbali, kuliombea taifa letu.
Kuwaombea wote wenye madaraka ili wajaliwe hekima, busara na upendo kwa taifa
na watu wake.
Kupitia jumuia ndogo ndogo na sharika zote,
waombee viongozi wetu ili Mungu awajalie na kuwatunuku kiu ya kutenda haki,
kusikiliza kuliko kusema, kuelekeza kuliko kuamrisha, kuunganisha kuliko
kutawanya, kupenda watu kuliko kutamani kupendwa na watu, kutamani kutumika kuliko
kutumikiwa (Marko 10:45), kuheshimu kuliko kuheshimiwa.
Ujumbe wa Pasaka unatuhimiza kuthamini uhai.
Bwana wetu Yesu Kristo alikubali kufa ili kuhifadhi uhai wetu. Kwa kufa kwake
na kufufuka, amekomesha kifo na mawakala wake. Tunaitwa kuthamini uhai na kutoruhusu
tena watu kuteswa na kuuawa.
Kwa hekima yote na unyenyekevu, tunasihi
tena, kwamba ikubalike kuwa hitaji la watanzania walio wengi kwa sasa ni KATIBA
MPYA. Katiba Mpya ipatikane ili kukuza na kuimarisha mfumo wa utawala
utakaolinda uhai wa watu, raslimali za nchi, tunu za taifa, uhuru wa mihimili
ya dola, na uwajibikaji wa viongozi kwa wananchi.
Tunawatakia Pasaka njema ya mwaka 2018, na
Mungu awabarikini nyote
SOMA WARAKA WA MAASKOFU 27 WA KKKT AMBAO UMEELEZA HALI YA NCHI ILIVYO.
Reviewed by KUSAGANEWS
on
March 24, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment