JESHI
la Polisi Mkoa wa Iringa jana lilimsafirisha mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam (UDSM) aliyedai kupotea mapema wiki hii, Abdul Nondo (24) kwenda
jijini Dar es Salaam kwa ajili ya uchunguzi.
Nondo ambaye ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi Tanzania
(TSNP), alidaiwa kutoweka kitatanishi usiku wa kuamkia Jumatano kabla ya juzi
kupatikana akiwa mkoani Iringa.
Akizungumza kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi
mkoa wa Iringa, Kamishna Msaidizi wa Polisi Juma Makanya alisema wamemsafirisha
kwenda jijini Dar es Salaam kwa mahojiano zaidi.
"Leo (jana) tumemsafirisha kwenda Dar es Salaam kwa ajili
ya uchunguzi zaidi kwa sababu huko ndipo alikotokea hadi kufika Iringa,"
alisema Kamanda Makanya.
Alisema Jeshi la Polisi linaendelea kumshikilia mwanafunzi huyo
kwa ajili ya uchunguzi zaidi wa kufahamu sababu ya tukio hilo.
Juzi Kamanda Makanya aliwaeleza waandishi wa habari kuwa Nondo
anayesoma mwaka wa tatu katika Kitivo cha Sayansi ya Siasa na Utawala cha UDSM,
aliripoti kwenye Kituo cha Polisi Mafinga wilayani Mufindi akiwa hana jeraha
lolote, akidai kutelekezwa na watu wasiojulikana.
Alisema Jeshi hilo linamchunguza ili kufahamu kama Nondo ametoa
taarifa za uongo kwa nia uovu ya kutaka kuhamasisha wanafunzi waandamane.
Kabla ya taarifa za kutoweka kwake, Nondo alizungumza na
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Jumanne na kumtaka Waziri wa Mambo ya
Ndani, Mwigulu Nchemba ajiuzulu nafasi kutokana na kupigwa risasi na kuuwawa
kwa aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina
Akwilin mwezi uliopita.
Akwilina, aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT),
aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa ndani ya daladala wakati wa maandamano ya
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jijini Februari 16.
Kutokana na mauaji hayo TSNP ilitoa tamko la kumtaka Mwigulu
ajiuzulu nafasi yake kuonyesha uwajibikaji kutokana na kile ambacho jumuiya
hiyo ilidai katika kipindi chake cha uongozi wizarani hapo, nchi imegubikwa na
matukio mengi ya mauaji na utekaji wa raia pamoja na Jeshi hilo kutozingatia
maadili yake ya kazi.
Baada ya kupotea, TSNP walitoa taarifa Kituo cha Polisi Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam na kufunguliwa jalada UD/RB/1438/2018.
Mwenyekiti wa TSNP asafirishwa kwenda Dar kwa uchunguzi zaidi.
Reviewed by KUSAGANEWS
on
March 10, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment