Baraza la Maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT), limetoa waraka mzito wa ujumbe wa Sikukuu ya Pasaka
ambao mbali ya kuzungumzia masuala ya kiroho, umetaja changamoto tatu na
kuzifikisha kwa waumini wake “ili ziongeze mzigo wa kuliombea taifa letu na
viongozi wake.”
Changamoto zilizotajwa katika waraka huo
uliopewa jina la ‘Taifa Letu Amani Yetu’ na kusainiwa na maaskofu 27 wa kanisa
hilo nchini ni hali ya kijamii na kiuchumi, maisha ya siasa na masuala mtambuka
likiwamo suala la Katiba Mpya
“Katika kukaa pamoja na kuliombea taifa
letu, sisi maaskofu wa KKKT, tumetafakari na kubaini changamoto hizo. Kwa njia
ya salamu za Pasaka, tunaleta kwenu changamoto tatu ili ziongeze mzigo wa
kuliombea taifa letu na viongozi wake,” inasema sehemu ya waraka huo
Salamu hizo za Pasaka zimetokana na kikao
cha maaskofu hao kilichofanyika Machi 15 na waraka huo umepangwa kusomwa leo
katika makanisa yote ya KKKT nchini
Huo ni waraka wa pili kutoka kwa viongozi wa
dini baada ya Februari mwaka huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC),
kutoa ujumbe wa Kwaresma uliosaniwa na maaskofu 35 uliozungumzia masuala ya
kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Alipotafutwa kutoa maoni kwa niaba ya
Serikali kuhusu waraka huo, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi alijibu
kwa kifupi; “Ujumbe huu unahusu Pasaka. Tunawatakia Pasaka njema.”
Mkuu wa KKKT, Dk Frederick Shoo alipoulizwa
jana juu ya waraka huo alisema asingependa kuuzungumzia kabla haujasomwa
akidokeza kwamba anachofahamu ni kuwa leo katika sharika zote za kanisa hilo
nchini kutasomwa waraka wa maaskofu wa kanisa hilo
“Nijuavyo Jumapili kesho (leo) kwenye nyumba
za ibada zote kutasomwa Waraka wa Pasaka kutoka Maaskofu wa KKKT. Sitaki
kuuzungumzia kwa sasa mpaka usomwe,” alisema Dk Shoo ambaye pia ni Askofu wa
Dayosisi ya Kaskazini
Siasa na Jamii
Maaskofu hao wameipongeza Serikali kwa
jitihada inazofanya kuboresha maisha ya wananchi wakisema wameshuhudia nia
njema kuhusu uvunaji na umilikaji wa rasilimali za nchi kwa manufaa ya taifa
zima
“Tunapongeza jitihada za ukusanyaji wa kodi
ili kuiwezesha Serikali kugharamia huduma za jamii,” unasema waraka huo na
kuitaka Serikali kutambua kwamba sekta binafsi na mashirika ya dini ni wadau wa
maendeleo na si washindani wa Serikali katika kuchangia maendeleo ya Taifa
“Jitihada za makusudi na za mara kwa mara
zifanyike kuondoa dhana ya ushindani kati ya Serikali na wadau hawa ili
kuimarisha mahusiano mema kati ya Serikali na sekta binafsi
Pia ili mfumo wa ukusanyaji wa kodi uwe
endelevu, jitihada za kukusanya kodi ziendane na elimu kwa mlipa kodi.
Msisitizo wa uzalendo wa kulipa kodi uende sambamba na ustawi wa walipa kodi
katika shughuli zao za biashara,” unasema waraka huo
Maaskofu hao wamesema mivutano isiyo na tija
kati ya walipa kodi na mamlaka ya ukusanyaji wa kodi, inastawisha uadui unaopunguza
makusanyo na kujenga ushawishi wa rushwa
Kuhusu hali ya uchumi wa viwanda, maaskofu
hao wameshauri uendane na uwekezaji katika sekta ya kilimo maeneo ya vijijini
na kwamba kilimo na ufugaji vihusishwe katika viwanda
Maisha ya Siasa
Waraka wa maaskofu hao pia ulichambua hali
ya kisiasa nchini na kusema; “Kwa umoja wetu katika utume, tunatambua siasa
safi na uongozi bora kuwa ni misingi iliyoongoza maisha ya siasa katika taifa
letu
“Ujio wa vyama vingi mnamo 1992, haukuondoa
umuhimu wa misingi hii, bali ulipanua matumizi ya demokrasia iliyojengwa katika
uhuru wa mawazo. Taifa ni mkusanyiko wa taasisi na watu mbalimbali, wenye lengo
moja lakini kwa njia mbalimbali. Kutokana na wingi huu, taifa letu daima ni juu
ya vyama, taasisi na makundi
“Taifa huongozwa na katiba iliyo kiini cha
sheria zote. Taifa haliongozwi na ilani za vyama. Serikali haiongozwi na ilani
za vyama. Serikali huongozwa na katiba, sheria, kanuni na mapokeo mema (misingi
na tunu za taifa). Serikali husimamiwa na Bunge huru lililo sauti ya wananchi
Wamesema wananchi ndilo chimbuko la madaraka
ya Bunge na kwamba chombo hicho hakisimamiwi na ilani, chama chochote wala mtu
awaye yeyote
Wameeleza kwamba kwa umoja wao na kwa
nyakati za hivi sasa kuna matukio yaliyo kinyume na tunu na misingi iliyolilea
Taifa inayoshuhudiwa; “Baadhi ya matukio hayo ni hofu iliyojengwa katika
matukio halisi yakiwamo utekaji, utesaji, kupotea kwa watu, mashambulizi ya
silaha dhidi ya viongozi wa kisiasa, mauaji yenye mwelekeo wa kiitikadi,
vitisho, ubambikiziaji wa kesi, na matumizi mabaya ya vyombo vya dola dhidi ya
wananchi
Pia wanasema kumekuwa na kupungua kwa uhuru
wa kujieleza, kukusanyika, na kupata habari na kuelezea hofu yao kuwa hali
ikiendelea hivyo hata uhuru wa kuabudu unaweza kuwa shakani
Pia wameelezea kuwapo kwa dalili za kupungua
kwa uhuru wa Bunge, Mahakama na Tume ya Uchaguzi na kile walichodai kuwa ni
kudhoofishwa kwa Serikali za Mitaa wakisema kumekuwa na mazingira kukosekana
kwa haki na uhuru wa kuchagua na kuchaguliwa katika chaguzi mbalimbali wakisema
zipo ambazo zimegubikwa na ubabe, vurugu, hila na vitisho
Wametaja pia kuwapo kwa dalili za
utekelezaji wa mipango ya maendeleo wenye mwelekeo wa kiitikadi na kuonya kuwa
hatua hiyo itaimarisha ubaguzi wa kiitikadi na kukuza migawanyiko
“Udhalilishaji wa kauli njema isemayo
“Maendeleo hayana chama”. Udhalilishaji huu unafanyika kwa njia ya kutumia
fedha nyingi katika chaguzi ndogo zinazotokana na watu wanaobadili vyama ili
kuleta maendeleo. Tunajiuliza, kama maendeleo hayana chama, kwa nini mtu
anajiuzulu chama fulani, eti kwenda kuleta maendeleo katika chama kingine?
Mchezo huu unagharimu fedha nyingi na maisha ya watu wanaokufa, kujeruhiwa na
uharibifu wa mali,” unasema waraka huo na kusisitiza kuwa mambo hayo ni tishio
kwa umoja na amani ya nchi
Masuala Mtambuka
Katika masuala mtambuka maaskofu hao
wanasema, “Ukimya wa Kanisa katika masuala yanayoigusa jamii ni ukwepaji wa
wajibu wake. Lakini pia sauti ya Kanisa isiyomilikiwa na mtu isipokuwa Mungu
tu, ni chachu ya amani na matumaini.”
Wametaja baadhi ya masuala hayo waliyoeleza
kuwa yanagusa maisha ya watu kwa njia nyingi kuwa ni pamoja na mfumo wa elimu
na kusema, “Elimu ni kitovu cha ustawi wa Taifa, kisiwe kinachokonolewa
chokonolewa kila wakati. Sekta zote nchini hujenga mafanikio yake katika
mafanikio ya mfumo thabiti wa elimu
“Uwezeshaji wa vijana kupata mikopo ya elimu
ya juu uwe shirikishi na usiokuwa na ubaguzi kati ya wanafunzi wa vyuo binafsi
na wale wa Serikali; sayansi na sanaa; wazazi maskini na wenye nafasi; waliosoma
shule binafsi na wale wa shule za Serikali.”
Mbali ya elimu waligusia suala la usimamizi
wa sheria na utoaji haki na kuvitaka vyombo husika vionekane vinatenda haki
sawa kwa watu wote na makundi yote bila kuacha ishara za fadhila au kukomoana
“Matukio ya mauaji ya askari wetu, mauaji ya
raia, majaribio ya kuwaua wanasiasa, utekaji, na uteswaji visipochunguzwa na
kutolewa taarifa, ni shina la hofu na uchungu katika jamii. Jamii iliyojaa hofu
na uchungu, haiwezi kuwa na maendeleo wala kuwa na roho ya uzalendo,” unaeleza
waraka huo.
Waraka huo haukuacha kuzungumzia suala la
Katiba Mpya. Unasema mambo mazuri yanayofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano
yatadumu iwapo kutakuwa na Katiba Mpya
“Kiongozi mzalendo si mbadala wa Katiba Mpya
na Tanzania yenye amani na maendeleo ni tunda la itikadi zote za dini, makabila
na makundi yote chini ya Katiba Mpya.”
Maaskofu KKKT watoa waraka mzito unaotaja kinachokabili Nchi kwasasa
Reviewed by KUSAGANEWS
on
March 25, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment