AHUKUMIWA JELA MIAKA 2827 KWA KUPATIKANA NA HATIA YA MAKOSA 419

RAIA wa Kenya, Stanley Murithi amehukumiwa kulipa faini ya Sh. milioni 100 au kwenda jela kutumikia kifungo cha miaka 2,827 baada ya kupatikana na hatia ya makosa 419 ikiwamo kujipatia kwa njia ya udanganyifu zaidi ya Sh. milioni 900 na kutakatisha fedha.

Kadhalika mahakama hiyo imesema mshtakiwa atalipa faini hiyo kwa kila kosa na akishindwa akatumikie kifungo hicho jela.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi 16 wa Jamhuri na mmoja wa utetezi.
Hakimu Shaidi alisema Murithi ameshtakiwa mahakamani hapo katika makosa 419 na kwamba kosa la kwanza hadi 99 ni kughushi, kosa la 100 hadi 198 ni kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, na kosa la 199 hadi 297 kujipatia nyaraka kwa njia ya uongo.
 Pia, hakimu huyo alisema kosa la 298 hadi 396 ni utakatishaji fedha na kosa la 397 hadi 419 ni kughushi.
Hakimu Shaidi alisema katika kosa la kwanza hadi 99 mahakama inamuhukumu Murithi kwenda jela miaka 7 kwa kila kosa.
Katika kosa la 100 hadi 198 la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu mahakama imemuhukumu Murithi kwenda jela miaka 7 kwa kila kosa.
Pia kosa la 199 hadi 297 mshtakiwa amehukumiwa kwenda jela miaka 7 kwa kila kosa.
Katika kosa la 298 hadi 396, Hakimu Shaidi alisema amehukumiwa Murithi kulipa faini ya Sh. mil. 100 kwa kila kosa sawa na Sh. bil 9.9 ama aende jela miaka 6 kwa kila kosa

Pia kosa la 397 hadi 419 anahukumiwa kwenda jela miaka 7 kwa kila kosa.

"Mahakama hii imekutia hatiani katika makosa hayo 419, inakuhukumu kwenda jela miaka 7 kwa kila kosa; jumla itakuwa miaka 2,827 lakini adhabu itakwenda sambamba hivyo ukishindwa kulipa faini utatumikia miaka saba jela," alisema Hakimu Shaidi

Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa mshtakiwa alikuwa anakabiliwa na kosa la kutakatisha fedha, kwamba kati ya Februari 6 na 7, 2012 jijini Dar es Salaam alijihusisha katika muamala wa kuhamisha fedha ambazo ni Sh. mil 4.9 kwa njia ya udanganyifu.
Pia inadaiwa kati ya Aprili 30 na Mei 5, 2013 alihamisha kiasi cha Sh. mil 6.5 kwa njia ya udanganyifu.



AHUKUMIWA JELA MIAKA 2827 KWA KUPATIKANA NA HATIA YA MAKOSA 419 AHUKUMIWA JELA MIAKA 2827 KWA KUPATIKANA NA HATIA YA MAKOSA 419 Reviewed by KUSAGANEWS on March 21, 2018 Rating: 5

No comments: