Utafiti uliofanywa na wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma
(Udom) kuhusu sababu za mkoa wa Dodoma kufanya vibaya katika elimu umeanika
mambo kadhaa ikiwemo wazazi kuwashawishi watoto wao wasifanye vizuri katika
mitihani yao.
Akizungumza katika mkutano wa wadau wa elimu mkoani hapa leo
Februari 20, 2018 mmoja wa jopo la wahadhiri hao, Dk. Fransic William
amesema baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwashawishi watoto wao kuandika makorokoro
katika mitahani yao ya Taifa
“Katika baadhi ya shule tulikuta wanafunzi walikuwa
wanafanya vizuri katika mitihani mingine ya ndani ya shule lakini ikija katika
mitihani ya Taifa wanafanya vibaya,”amesema Dk William.
Amesema pia katika utafiti huo, walibaini pia kuna shule
zina madarasa matatu tu lakini wanafunzi wapo hadi darasa la saba na hivyo
kulazimika wengine kusoma na kukaa chini ardhini kwa ukosefu wa vyumba vya
madarasa na madawati
“Hao unaowaona wamelala hapo chini ndio wanafanya mitihani
hapo. Unakuta shule ina walimu wawili na wanafunzi 700 kwa wiki mwalimu
anavipindi 60 hapo unadhani anaweza kumudu kweli,”
amehoji.
Amesema pia tatizo jingine ni wanafunzi kulazimika kutembea
umbali mrefu kutoka na kurudi nyumbani ambapo kuna watoto wanatembea umbali wa
kuanzia kilometa tano hadi 18 kwa siku.
Ametoa mfano wa shule mojawapo kati ya watoto 9 waliokwenda
kula chakula cha mchana nyumbani waliorejea walikuwa wanne kwa ajili ya vipindi
vya mchana na wengine hawakuweza kurudi nyumbani kwa chakula cha mchana
kwasababu ya umbali.
Pia, amesema ratiba ya wanafunzi wa shule za msingi kuwa na
saa nyingi zaidi ya ile ya shule ya sekondari ambapo kwa sekondari ratiba ya
masomo huisha saa 8.30 mchana wakati ya msingi humalizika saa 9.30 mchana.
Ofisa wa Elimu Mkoa wa Dodoma, Maria Lyimo amesema wanafunzi
12,052 sawa na asilimia 22.23 walishindwa kumaliza darasa la saba mwaka 2017
kwa sababu ya utoro huku mwaka 2016 wakishindwa kumaliza 12,406 sawana asilimia
24.95.
SABABU YA WANAFUNZI KUFANYA VIBAYA KATIKA ELIMU DODOMA NI WAZAZI
Reviewed by KUSAGANEWS
on
February 20, 2018
Rating:

No comments:
Post a Comment