Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema
kuwa atawashughulikia wakuu wa wilaya ambao watashindwa kukomesha vitendo vya
wanafunzi wa kike kupewa mimba.
Amesema kuwa yeye kama kiongozi mkuu wa juu
mwanamke, atahakikisha anapambana na watu wote wanaowapa mimba watoto wa kike
wakiwa bado shuleni, huku akiwaonya madereva pikipiki (bodaboda).
Mama Samia ametoa kauli hiyo jana kwenye
mkutano wa hadhara wa wananchi uliofanyika katika viwanja vya Nguzo Nane mjini
Maswa mkoani Simiyu.
Amesema atahakikisha anawashughulikia
wakuu wa wilaya wote nchini ambao hawataonyesha jitihada zao za kuhakikisha
wanapambana na wale wote wanaowapa mimba watoto wa kike
“Mimi kama kiongozi wa juu mwanamke ni
lazima macho yangu yawe makini kuangalia na kuwashughulikia wale wote ambao
wanawaharibia malengo kusudiwa watoto wa kike…na kuonyesha kuwa niko
makini nitaanza na wakuu wa wilaya wasiowajibika na hilo,’’ amesema Mama Samia.Amesema kuwa
serikali haiwezi kuwafumbia macho wale wote wanaoharibu maisha ya watoto wa kike halafu wakaachwa tu bila sheria kali kuchukuliwa dhidi yao.
Aliongeza kuwa Serikali yake imekuwa
ikijitahidi kutoa fedha nyingi kila mwezi katika sekta ya elimu
ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bure hivyo hatarajii kuona watoto wa
kike wanaishia njiani pasipo kutimiza ndoto zao
Awali akimweleza Makamu wa Rais Mkuu wa
Wilaya ya Maswa Dkt Seif Shekilage alisema wilaya yake imekuwa na tatizo kubwa
la mimba kwa watoto wa kike na kwa kipindi cha Desemba 2017 hadi sasa tayari
matukio ya mimba yamefikia 20
Shekilage amesema kati ya kesi 20
zilizofunguliwa kesi mbili tayari zimeshatolewa hukumu na watuhumiwa wamefungwa
kifungo cha miaka 30 jela
Dk Shekilage amesema kuwa wilaya yake
imekuwa ikijitahidi kuhakikisha tatizo la mimba linaisha kwa kutoa elimu kwa
watoto wa kike na jamii ikiwa sambamba na kuwachukulia wale wanaobainika kuwapa
mimba wanafunzi
“Katika wilaya yangu tunajitahidi
kuhakikisha suala la mimba tunalipunguza…mimi binafsi nafuatilia sana wale
waharibifu wanaoharibu maisha ya watoto wa kike,’’ amesema
Pia amemuhakikishia Makamu wa Rais kupambana
na wote wanaowaharibia wanafunzi maisha yao kwa kuwapa mimba ili watoto hao wa
kike waweze kufikia malengo.
Akiwa wilayani Itilima Makamu wa Rais
aliahidi kujenga hospitali ya wilaya, ambapo Mbunge wa Jimbo hilo Njalu Silanga
(CCM) alisema ukosefu wa hospitali hiyo umekuwa kero kwa wananchi wake.
MAKAMU WA RAISI AAHIDI KUSHUGHULIKIA WAKUU WA WILAYA
Reviewed by KUSAGANEWS
on
February 21, 2018
Rating:

No comments:
Post a Comment