Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amempa wakati
mgumu Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela, John Wanga baada ya kumtaka atoe jibu
la papo hapo kuhusu lini wakazi wa eneo la Mhonze wilayani Ilemela watalipwa
fidia ya ardhi yao waliyozuiwa kuiendeleza.
Hatua hiyo ya Waziri Mkuu imetokana na
kitendo cha wakazi wa eneo hilo kumpokea kwa mabango wakilalamikia kutolipwa
fidia kwa muda mrefu licha ya ardhi yao kufanyiwa tathmini na Manispaa ya
Ilemela wakitakiwa kuhama kwa ajili ya usalama wa Uwanja wa Ndege Mwanza
"Kama tayari tathmini imefanyika na
wananchi kuzuiwa kuendeleza maeneo yao, kwanini hamuwalipi fidia ili waondoke?
Mkurugenzi nataka majibu ya kueleweka hapa hapa,” Waziri Mkuu akadai majibu
kutoka kwa Wanga
Bila kutaja lini wananchi hao watalipwa
fidia, Wanga (huku wananchi wakiguna), akasema malipo yamecheleweshwa na
kitendo cha baadhi ya wakazi wa eneo hilo kuendeleza maeneo yao baada ya zoezi
la tathmini
“Sitaki majibu ya kuzungukazunguka; je, fedha
za kulipa fidia zipo na ni lini wananchi hawa watalipwa?” akasisitiza swali
Waziri Mkuu na kuibua shangwe kutoka kwa wananchi
Swali hilo likaonekana gumu kwa Wanga na
kuomba msaada kwa ofisa ardhi (jina halikujulikana mara moja), ambaye pia
akalikwepa kwa kusema ana muda mfupi tangu alipoanza kazi Manispaa ya Ilemela,
hivyo hawezi kujua iwapo fedha zipo hadi apitie nyaraka.
Mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella
amelazimika kuingilia kati kuokoa jahazi kwa kuahidi kuwa suala hilo
litashughulikiwa na kumalizika ndani ya kipindi cha miezi mitatu, jibu
lililomridhisha Waziri Mkuu
“Angalau kidogo maelezo ya mkuu wa mkoa
nayaelewa; kwa hiyo wananchi tusubiri huo muda alioahidi mkuu wa mkoa,”
Majaliwa akawaeleza wananchi waliolipuka kwa shangwe
Akizungumzia kero na migogoro ya ardhi
nchini, Waziri Mkuu amesema nyingi ni matokeo ya watendaji wa halmashauri
kutumia muda mwingi kukaa maofisini badala ya kwenda kwa wananchi kusikiliza na
kutatua kero zao
“Nimeshaagiza maofisa ardhi wote nchini
waende kwa wananchi kusikiliza na kutatua matatizo na kero za ardhi; utatuzi wa
kero na migogoro ya ardhi itakuwa miongoni mwa vigezo vya kupima utendaji na
uwajibikaji,” amesema Majaliwa.
Majaliwa Amtaka mkurugenzi kutoa jibu la papo hapo kuhusu mgogoro
Reviewed by KUSAGANEWS
on
February 21, 2018
Rating:

No comments:
Post a Comment