WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amemaliza mgogoro wa matumizi ya pori tengefu la Loliondo ambao umedumu kwa
takriban miaka 26.
Hatma hiyo imefikiwa jana (Jumatano,
Desemba 6, 2017) kwenye kikao kilichoitishwa na Waziri Mkuu ofisini kwake
Mlimwa, Manispaa ya Dodoma ili kutoa mrejesho uliofikiwa na Serikali kuhusu
utatuzi wa mgogoro huo baada ya kupokea taarifa ya Kamati ya Uchunguzi.
Waziri Mkuu alisema Serikali
imekubali mapendekezo ya kuunda chombo maalum kitakachosimamia eneo la Loliondo
ili kunusuru ikolojia ya Hifadhi ya Serengeti na kulinda mazingira na eneo
mahsusi la mazalia ya wanyamapori, mapito na vyanzo vya maji.
“Baada ya kupitia mifumo mbalimbali,
timu ya wataalam ilipendekeza kuwa utumike mfumo maalum utakaounda chombo
maalum, kwa kuwa una maslahi mapana kwa pande zote husika na unalenga kuleta
amani na kufikia lengo la kuwa na uhifadhi endelevu katika eneo la Loliondo,”
alisema.
Waziri Mkuu aliiagiza Wizara ya
Maliasili iandae muswada wa kutunga sheria mahsusi ya kuwa na chombo maalum au mamlaka
ya kusimamia eneo la Loliondo ili kunusuru ikolojia ya Hifadhi ya Serengeti
pamoja na kulinda mazingira na eneo mahsusi la mazalia ya wanyamapori, mapito
na vyanzo vya maji kwa ajili ya ustawi wa hifadhi muhimu zenye maliasili na
rasilimali za Taifa kwa manufaa ya wananchi wenyewe na Taifa kwa ujumla.
“Sheria itakayotungwa ihakikishe
inawekewa masharti yanayozingatia maslahi ya jamii iliyopo katika eneo la
Loliondo, mila zao na desturi zao pamoja na mahusiano yao na matumizi ya
ardhi,” alisisitiza Waziri Mkuu na kushangiliwa na wajumbe zaidi ya 60
waliohudhuria kikao hicho.
Vilevile, Waziri Mkuu aliiagiza
Wizara ya Maliasili na Utalii iandae waraka maalum utakaowasilishwa Serikalini
kupitia Baraza la Mawaziri kuhusu umuhimu wa kutunga sheria mahsusi ya eneo la
Loliondo.
Alisema kuna ulazima wa kushirikisha
wadau wote mara baada ya rasimu ya kwanza kukamilika ili wadau waipitie kwanza.
Alisisitiza rasimu ya pili iwe imefanyiwa mapitio na kukamilika ifikapo
Februari au Machi, 2018 ili mahitaji ya fedha yaingizwe kwenye mchakato wa
Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2018/2019.
Aliwataka Waheshimiwa Mawaziri na
Makatibu Wakuu wa Wizara za Kisekta zinazohusika na mgogoro wa matumizi ya
ardhi ya Pori Tengefu la Loliondo wafanye ziara ya kutembelea eneo hilo ili
wawe na uelewa mpana kuhusu changamoto za kisekta zilizopo katika eneo husika.
Kikao hicho kilihudhuriwa na
Mawaziri wa Maliasili na Utalii; TAMISEMI; Ardhi na Maendeleo na Makazi; Naibu
Mawaziri wa Kilimo; Maji; Mifugo na Uvuvi na Elimu na Mafuzo. Pia kilihudhuriwa
na wakuu wa taasisi za Serikali, wawekezaji walioko Loliondo, uongozi wa mkoa
wa Arusha, madiwani na wananchi kutoka Loliondo.
Desemba 2016, Waziri Mkuu alifanya
ziara ya kikazi wilayani Ngorongoro ambako alipokea taarifa ya kuwepo mgogoro
wa matumizi ya ardhi katika Pori Tengefu la Loliondo. Januari 2017, aliunda
Kamati ya Uchunguzi iliyokuwa na wajumbe 27 ambayo iliongozwa na Mkuu wa Mkoa
wa Arusha, Bw. Mrisho Gambo.
Washiriki wa kikao hicho waliopata
fursa ya kutoa maoni, walipongeza uamuzi wa Serikali ya awamu ya tano wa
kuwashirikisha wananchi hadi ngazi ya chini katika kutafuta suluhu la mgogoro
huo.
Akichangia kwa niaba ya NGOs,
Mkurugenzi wa taasisi isiyo ya Kiserikali ya Pastoralist Women Council, Bi.
Manda Neritiko aliishukuru Serikali kwa kuwashirikisha wananchi kutafuta suluhu
ya mgogoro huo, hatua ambayo alisema haijawahi kufanyika miaka yote ya nyuma.
“Huko nyuma tulikuwa tukipewa
maagizo tu, Serikali imeamua hivi, Serikai imesema vile, lakini kwa awamu hii,
tumeweza kuitwa kwenye vikao mbalimbali na kutoa maoni yetu na hata kupewa
mrejesho,” alisema.
Aliomba hata katika chombo kipya
kitakachoundwa, kuwe na uwakilishi wa wananchi kutoka ngazi ya chini ili waweze
kushiriki kikamilifu katika kupanga namna bora ya kuendeleza eneo hilo.
Kwa upande wa wawekezaji, Bw. Scott
Tineja Mollel kutoka kampuni ya AndBeyond Tanzania, alisema wao kama wawekezaji
wanataka kuhakikishiwa kuwepo kwa utalii wa kesho. “Hatuwezi kuwa na utalii wa
kesho kama hatutunzi mazingira ya sasa,” alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
Waziri Mkuu Amaliza Mgogoro Wa Loliondo
Reviewed by KUSAGANEWS
on
December 07, 2017
Rating:

No comments:
Post a Comment