Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma katika Ikulu ya Chamwino Mkoani
Dodoma.
Baada ya mazungumzo hayo Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema Mhe. Rais Magufuli amemuahidi kuwa Serikali itatoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa Mahakama Kuu Mkoani Dodoma na kwamba ujenzi wa majengo utaanza mwezi ujao.
Ameongeza kuwa ujenzi huo utakuwa ni
wa Makao Makuu ya Mahakama na Mahakama ya Rufani, na pia utaambatana na ujenzi
wa makazi ya Majaji.
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma
ameongeza kuwa pamoja na kuanza kwa ujenzi huo Mkoani Dodoma Mahakama
inaendelea na ujenzi wa majengo ya Mahakama Kuu katika Mikoa ya Mara, Kigoma,
Morogoro na Singida.
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma
amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa ushirikiano wake kwa Mahakama na ameahidi
kuwa Mahakama itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi na ufanisi zaidi
ikiwemo kupunguza msongamano wa mashauri mahakamani.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
IKULU
Chamwino, Dodoma
07 Desemba, 2017
Rais Magufuli akutana na Jaji Mkuu wa Tanzania Dodoma
Reviewed by KUSAGANEWS
on
December 07, 2017
Rating:

No comments:
Post a Comment