Watu watatu wanaodaiwa
kuwa majambazi wameuawa kwa kupigwa risasi na polisi mkoani Kilimanjaro.
Kamanda wa Polisi Mkoa
wa Kilimanjaro, Hamis Issah amesema watu hao waliuawa Jumanne Desemba 5,2017
jioni katika msitu wa Njoro wakati wa majibizano ya risasi na polisi.
Amesema watuhumiwa hao
wa ujambazi walikuwa wakiishi chumba kimoja eneo la Njoro ambako polisi
walipofika hawakuwakuta na walipata taarifa kuwa wamejificha msituni.
Kamanda Issah amesema
kwa kushirikiana na wananchi walikwenda ndani ya msitu huo ambako walisikia
milio ya risasi ndipo askari walipofyatua risasi na kusababisha vifo vyao.
Amewataja waliouawa
kuwa ni Yusufu Juma Mdoe aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya mauaji mwaka 2015;
Francis Hamis Kinyaia ‘Wakudata’ ambaye amesema alikuwa akikabiliwa na kesi ya
mauaji mwaka 2013.
Kamanda Issah amemtaja
mwingine kuwa ni Valerian Joackim ‘Mdoe’ aliyekuwa na kesi ya mauaji ya mwaka
2013.
Amesema uchunguzi wa
polisi umebaini watuhumiwa hao walihusika katika tukio la kufungwa miguu,
mikono na kuzibwa mdomo mlinzi lililotokea Novemba 24,2017 eneo la Uru Shimbwe.
Katika tukio hilo, bunduki mbili aina ya shotgun ziliporwa.
Kamanda Issah amesema
katika msitu wa Njoro walikuta bunduki moja aina ya shotgun iliyokatwa mtutu na
kitako, huku namba zikiwa zimefutwa, risasi tatu, maganda matatu ya risasi,
mapanga mawili, mkasi unaotumika kukata makufuli, kirungu cha polisi, tindo na
misokoto miwili ya bangi.
Ameema miili ya
watuhumiwa imehifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Kilimanjaro ya
Mawenzi.
Watuhumiwa watatu wauawa kwa risasi na Polisi Kilimanjaro
Reviewed by KUSAGANEWS
on
December 06, 2017
Rating:

No comments:
Post a Comment