“Jioni hii nimepokea
kwa mshtuko na huzuni kubwa taarifa za kifo cha Mkuu wa Mkoa Mstaafu Dkt. Joel
Nkaya Bendera, natoa pole kwa familia yake na wote walioguswa na msiba huu na
pia naungana nao katika kipindi hiki cha majonzi”
Hii ni sehemu ya
salamu za rambirambi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John
Pombe Magufuli alizozitoa kufuatia kifo cha aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara
Dkt. Joel Nkaya Bendera kilichotokea jioni ya leo tarehe 06 Desemba, 2017
katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam alikofikishwa kwa
ajili ya kupata matibabu.
Mhe. Rais Magufuli
amesema Dkt. Joel Bendera atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa alioutoa kwa
Taifa akiwa kiongozi katika nyadhifa mbalimbali zikiwemo Mkuu wa Mkoa wa
Manyara, Naibu Waziri na Mbunge na pia kwa mchango wake mkubwa katika maendeleo
ya michezo.
“Dkt. Joel Nkaya
Bendera alikuwa kiongozi shupavu, mahiri na mchapakazi, alipenda kufanya kazi
kwa ushirikiano na daima alitamani kupata mafanikio makubwa katika majukumu
aliyokuwa nayo, hakika tutamkumbuka” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Pamoja na kutoa pole
kwa familia ya marehemu, Mhe. Rais Magufuli amewapa pole wananchi wa Mkoa wa
Manyara ambako alikuwa Mkuu wa Mkoa hadi tarehe 26 Oktoba, 2017, wananchi wa
Mkoa wa Tanga ambako alikuwa Mbunge, wanachama wote wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM), Wanamichezo wote na wote walioguswa na msiba huu na amemuombea kwa
Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake mahali pema peponi, Amina.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa
Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
06 Desemba, 2017
Rais Magufuli aomboleza kifo cha aliyekuwa RC Manyara
Reviewed by KUSAGANEWS
on
December 06, 2017
Rating:

No comments:
Post a Comment