Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma itatoa uamuzi wa maombi ya
dhamana ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Sadifa Juma
Khamis anayekabiliwa na makosa ya rushwa Desemba 19,2017.
Uamuzi huo unatokana na upande wa mashtaka kuwasilisha hati
ya kiapo kuzuia dhamana kwa madai ya kuvurugwa upelelezi na kuingilia uchaguzi
wa UVCCM ambao ulifanyika jana Jumapili Desemba 10,2017 na leo Jumatatu
Desemba 11,2017 katika ukumbi wa Chuo cha Mipango mjini Dodoma.
Akisoma hati ya mashtaka mahakamani, Wakili wa Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Biswalo Biswalo amedai Sadifa
anashtakiwa kwa makosa mawili
Katika shtaka la kwanza amedai Desemba 9,2017 katika makazi
yake kwenye Kata ya Mnada mjini Dodoma akiwa mwenyekiti wa Taifa wa UVCCM na
muajiri wa umoja huo aliwahonga wanachama ili wamchague Rashid Mohamed
aliyekuwa akiwania nafasi ya makamu mwenyekiti katika uchaguzi mkuu wa umoja
huo
Sadifa katika shtaka la pili anadaiwa katika eneo hilo na
siku hiyohiyo, aliwaahidi kuwalipia usafiri wanachama wa umoja huo
kuwasafirisha kutoka Dodoma hadi Kagera kama zawadi ili wamchague Rashid
Mohamed aliyekuwa akiwania nafasi ya makamu mwenyekiti katika uchaguzi huo
Biswalo amesoma hati ya kiapo iliyotolewa na Kamanda wa
Takukuru Mkoa wa Dodoma, Emma Kuhanga kupinga maombi ya dhamana kwa sababu
endapo atapewa dhamana atavuruga upelelezi na kuingilia uchaguzi wa vijana
Wakili wa Utetezi, Godfrey Wasonga amepinga hoja hiyo
akisema makosa aliyoshtakiwa nayo mteja wake yana dhamana na hawezi kuingilia
uchaguzi kwa kuwa umeshafanyika na mshindi ametangazwa.
Kutokana na mabishano hayo, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya
Hakimu Mkazi Dodoma, Emmanuel Fovo ameahirisha kesi hiyo hadi Desemba 19,2017
kutoa nafasi ya mahakama kupitia kiapo kilicholetwa na upande wa mashtaka ili
kutoa haki katika maombi ya dhamana ya mshtakiwa.
Kutokana na hilo, Sadifa amerejeshwa rumande.
Mwenyekiti wa UVCCM Sadifa Juma Apandishwa kizimbani na Kusomewa mashtakiwa mawili.
Reviewed by KUSAGANEWS
on
December 11, 2017
Rating:

No comments:
Post a Comment