Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
kesho Ijumaa inatarajiwa kutoka uamuzi katika kesi ya uhujumu uchumi
inayomkabili aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani
Madabida na wenzake watano kama ina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo ama
la.
Uamuzi huo unatarajiwa kutolewa na
Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa.
Utatolewa baada ya kusikilizwa hoja
zilizowasilishwa na upande wa mawakili wa Serikali, Pius Hilla na Shedrack
Kimaro na mawakili wa utetezi, Denis Msafiri, Makaki Masatu na Nehemia Nkoko.
Wakili wa Serikali, Kimaro
akiwasilisha hoja zao leo Alhamisi alidai kuwa hoja ya mawakili wa utetezi kuwa
Mahakama ya Kisutu ina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo kwa sababu ipo chini ya
Sh 1 bilioni siyo sahihi.
Amedai kuwa ni dhahiri kuwa makosa
hayo ni ya uhujumu uchumi na mamlaka yenye mamlaka ya kuisikiliza ni Mahakama
Kuu Kitengo cha Rushwa na Uhujumu Uchumi maarufu Mahakama ya Mafisadi.
“Hivyo mahakama za chini kama
Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo labda kuwepo na
kibali cha kulipa mamlaka ya kuisikiliza kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka
(DPP).”
Kutokana na hilo aliiomba Mahakama
kutupilia mbali hoja za upande wa utetezi.
Wakili wa utetezi, Msafiri alidai
kuwa ameusikia upande wa mashtaka, ila ni rai yao kuwa marekebisho ya sheria ya
uhujumu uchumi ya 2016 yanaipa moja kwa moja Mahakama ya Kisutu kuisikiliza
kesi hiyo.
Alidai kuwa kosa lolote lililopo
chini ya Sh 1 bilioni haliwezi kusikilizwa na Mahakama Kuu Kitengo cha Rushwa
na Uhujumu Uchumi ni Mahakama za chini ikiwamo Mahakama ya Kisutu.
Alisisitiza kuwa Mahakama ya Kisutu
ina mamlaka kamili ya kuisikiliza kesi hiyo kwa vile shtaka halizidi Sh 1
bilioni na kwamba mahakama hiyo ndiyo yenye mamlaka ya kuisikiliza kesi hiyo na
siyo Mahakama Kuu.
Pia alidai kuwa kibali cha DPP cha
kuipa mamlaka mahakama kusikiliza kesi kinapaswa kipelekwe mahakamani pamoja na
hati ya mashtaka.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi kesho
Ijumaa ambapo mahakama itatoa uamuzi na washtakiwa waliamuliwa wapelekwe
polisi.
Hata hivyo, Wakili wa Serikali, Pius
Hilla aliomba wapelekwe magereza kwa sababu washtakiwa hao kuendelea kuwa
mikononi mwa polisi kuna suala la gharama na polisi hawana fungu.
Baada ya kutolewa kwa ombi hilo,
Wakili Nkoko aliomba Mahakama kusimamia amri yake kama ilivyoitoa.
Wakili Masatu naye aliiomba mahakama
iendelee na oda yake ilivyoitoa jana Jumatano.
Hakimu Nongwa amesema suala la
gharama hawawezi kulikwepa pale haki inapotafutwa na kuamuru washtakiwa
wapelekwe polisi hadi kesho Ijumaa atakapotoa uamuzi kama mahakama hiyo ina
mamlaka ama la.
Madabida na wenzake wanakabiliwa na
mashtaka sita ya uhujumu uchumi ikiwamo kusambaza dawa bandia za kufubaza
virusi vya Ukimwi ' ARV’s ' na kusababisha hasara ya Sh 148 milioni.
Mvutano waibuka kesi ya Madabida na wenzake....Mahakama kutoa uamuzi leo
Reviewed by KUSAGANEWS
on
December 07, 2017
Rating:

No comments:
Post a Comment