Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif
Sharif Hamad, ameungana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli, katika kuomboleza vifo vya askari 14 waliouawa nchini Kongo na
wengine kujeruhiwa, huku akiwapa pole wafiwa wote.
Kufuatia msiba huo Maalim Seif
ametuma salamu za rambirambi kwa Rais Magufuli, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali
Venance Salvatory Mabeyo, Maafisa na Askari wote wa JWTZ, familia na ndugu wa
marehemu na Watanzania wote kwa ujumla, kwa kuwapoteza mashujaa waliokuwa
wakitekeleza wajibu wao kwa niaba ya Taifa.
"Natuma salamu zangu za
rambirambi kwa ndugu, jamaa na marafiki wa waathirika wote na Amiri Jeshi Mkuu
wa Majeshi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na kwa wale waliojeruhiwa
nawatakia uponaji wa haraka ili warejee katika majukumu yao ya kawaida, na
tunawaombea marehemu wote Mwenyenzi Mungu awapumzishe mahala pema peponi",
amesema Maalim Seif.
Pamoja na hayo Maalim Seif amesema
anaungana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kulaani shambulio hilo, na kuitaka
nchi ya Congo kufanya uchunguzi juu ya tukio hilo, na kuwachukulia hatua wale
waliohusika.
“Tunaungana na Katibu Mkuu wa Umoja
wa Mataifa Antonio Guterres kulaani shambulio hilo ambalo ni sawa na uhalifu wa
kivita, na kuitaka DRC Congo kufanya uchunguzi kuhusu shambulio hilo na
wahusika wote kuchukuliwa hatua stahiki na kuwajibishwa", amesema Maalim
Seif.
Hapo Jana imetolewa taarifa kuwa
askari 14 wa Tanzania wa kulinda amani nchini Kongo wameuawa, huku 44 wakiwa
majeruhi, 8 miongoni mwao wakiwa mahututi, na wawili hawajulikani walipo.
Maalim Seif aungana na Rais Magufuli katika maombolezo ya Askari 14 waliouwawa Kongo
Reviewed by KUSAGANEWS
on
December 09, 2017
Rating:

No comments:
Post a Comment