UHURU AREJEA UKAMBANI, AMTAKA RAILA PIA 'AIBE KURA'

RAIS Uhuru Kenyatta, Alhamisi alirejea katika eneo la Ukambani kuomba kura, siku moja baada ya kusema atashinda bila kura za jamii hiyo. 

Tofauti na matamshi yake ya awali yaliyoonekana kupuuza kura za Ukambani, jana alisihi wakazi wa eneo hilo wampigie kura kwa wingi ili amshinde mpinzani wake wa karibu, Bw Raila Odinga wa Muungano wa NASA, kwa pengo kubwa.

“Njooni tuhakikishe tumemshinda kwa kura nyingi ili aache hizi stori zake za kudai ameibiwa kura,” akasema akiwa Mwingi, Kaunti ya Kitui.

Kaunti hiyo yenye wapigakura 474,512 huchukuliwa kuwa ngome ya Kiongozi wa Chama cha Wiper Bw Kalonzo Musyoka, ambaye ni mgombea mwenza wa Bw Odinga.

Eneo hilo ni miongoni mwa yale yanayotegemewa pakubwa na NASA kupata ushindi katika uchaguzi wa urais utakaofanywa Jumanne wiki ijayo.

Baadaye alipohutubu akiwa mjini Kitui, rais alitoa changamoto kwa Bw Odinga, aibe kura kama kweli anaamini yeye huibiwa kila mara.

Pia wewe iba

“Kila mwaka akiingia uchaguzini anasema ameibiwa...sasa wewe kama unaibiwa kila mara shida ni nani? Pia wewe si uibe,” akasema rais.

Kulingana na rais, Kiongozi huyo wa Chama cha ODM alipoteza muda mwingi kwenye vikao vya wanahabari kudai jeshi litatumiwa kuiba kura, na mahakamani kupinga baadhi ya mipango ya kuandaa uchaguzi wakati Jubilee ilipokuwa ikijipigia debe kwa hivyo inafaa atarajie kushindwa.

Kwa upande wake, naibu wa rais alisema Jubilee haitaweza kuunda serikali bila kura za watu wa Kaunti ya Kitui.

Walipokuwa Mwingi, Bw Ruto, aliambia Wakenya wasitarajie wizi wowote wa kura katika uchaguzi mkuu wa wiki ijayo.

“Hakutakuwa na wizi. Wananchi wa Kenya watapiga kura Agosti 8 na kuamua wale watakaokuwa viongozi wao,” akasema.

Mbali na Kitui na Mwingi, wawili hao walihutubia mikutano ya hadhara katika Kaunti ya Meru na Tharaka Nithi.

Miraa

Akiwa Meru, Rais Kenyatta alitoa wito kwa viongozi wa Chama cha Biashara ya Miraa cha Nyambene washauriane na serikali ili kesi inayozuia utumizi wa Sh1 bilioni za kusaidia wakulima wa miraa iondolewe kwa manufaa ya wakulima.

“Serikali imetoa pesa lakini kesi imekaa kortini. Ninaomba kwa heshima kubwa waondoe hiyo kesi ili pesa zifikie wananchi. Kama kuna tatizo tutatue hapa,” akasema.

Viongozi hao walisihi wapigakura kuwachagua ili wapate nafasi ya kuendeleza miradi ya maendeleo huku wakieleza kuhusu mipango yao endapo watachaguliwa kuongoza kwa miaka mitano ijayo.

Waliorodhesha mafanikio waliyoleta katika maeneo waliyozuru kama vile ujenzi wa barabara, usambazaji wa umeme, uboreshaji wa huduma za afya miongoni mwa mengine.

Waliahidi kukamilisha miradi iliyokwama kama wakazi watawachagua kuunda serikali ijayo.

UHURU AREJEA UKAMBANI, AMTAKA RAILA PIA 'AIBE KURA' UHURU AREJEA UKAMBANI, AMTAKA RAILA PIA 'AIBE KURA'


Reviewed by KUSAGANEWS on August 03, 2017 Rating: 5

No comments: