MKE wa Mgombeaji Urais wa Muungano wa NASA Bw Raila Odinga, amemkosoa Naibu wa Rais William Ruto, kwa kukejeli vitendawili vya kinara huyo wa upinzani kila mara.
Bi Ida Odinga, alisema vitendawili vinavyotumiwa na mume wake katika mikutano ya hadhara ni kati ya mambo yaliyompa Bw Ruto umaarufu kisiasa alipokuwa katika chama kimoja na Bw Odinga mwaka wa 2007, na kumfikisha mahali aliko Ijumaa.
“Vitendawili ni vizuri. Unapohutubia watu, wanaweza kusahau yale unawaambia kirahisi. Lakini ukitumia vitendawili na hadithi watakumbuka. Ruto nafaa ashukuru kwa vitendawili,” akasema.
Bi Odinga alikuwa akizungumza kwenye mahojiano aliyofanyiwa Jumatano usiku katika runinga ya NTV.
“Nimeona viongozi ambao kazi yao ni kuonya tu, kila mara wakisimama jukwaani tunajua wanaenda kutuonya na kunyosha vidole na kuchochea wengine. Huo si uongozi. Pitisha ujumbe wako kwa njia ya kirafiki,” akasema.
Bw Ruto amekuwa na mazoea ya kuuliza wananchi kama wanataka kuongozwa na “yule mtu wa vitendawili” wakati mwingi anapohutubia mikutano ya hadhara.
Katika mahojiano hayo, Bi Odinga alifichua kuwa mume wake alijifunza mafumbo, hadithi na vitendawili alipofungwa gerezani katika enzi za utawala wa Rais Mstaafu Daniel arap Moi.
Kulingana naye, Bw Odinga hakuwa na chochote kingine cha kufanya alipokuwa gerezani ila kusoma, na hata akasoma Biblia nzima mara tatu.
Alieleza matumaini yake kuwa NASA itashinda urais wiki ijayo, lakini akasema hata wakishindwa haitamaanisha ni “mwisho wa ulimwengu” huku akitoa wito kuwe na uchaguzi huru, wa haki na kuaminika.
Bi Odinga alisema ana maono ya kusaidia wasichana zaidi kupata elimu, kuboresha huduma za matibabu kwa umma na kusaidia kina mama wasio na waume.
“Kina mama wasio na waume hawajashughulikiwa ipasavyo kwani wameachwa kushindana na kila mtu katika jamii,” akasema.
Ari yake ya kusaidia kundi hilo la wanawake katika jamii ni kutokana na yale aliyopitia wakati mume wake alipofungwa gerezani akabaki na watoto wanne.
“Ilikuwa wakati mgumu, mara nyingi tulikuwa peke yetu. Haikudumu milele lakini nilikuwa peke yangu kwa karibu miaka 10. Haikuwa rahisi kutunza watoto na wakati huo huo nina hofu kuhusu mume wangu aliye gerezani,” akasema.
Aliongeza kwamba akiwa Mama wa Taifa haitakuwa nafasi ya kustarehe bali kuchangia kuleta mabadiliko katika jamii, huku akitoa wito wanawake wawezeshwe kutumia uwezo na maarifa yao ipasavyo kuchangia katika maendeleo ya taifa.

No comments:
Post a Comment