MSANDO NA CAROL NGUMBU WALINYONGWA HADI KUFA - MPASUAJI

CAROL Ngumbu, ambaye mwili wake ulipatikana karibu na ule wa meneja wa masuala ya teknolojia katika tume ya uchaguzi, Bw Chris Msando, alinyongwa hadi kufa.

Mpasuaji Maiti wa Serikali Alhamisi alisema Bi Ngumbu, 21, alinyongwa kwa kutumia kamba.

“Alikufa baada ya kunyongwa koo kwa kamba,” alisema mpasuaji huyo Dkt Johansen Oduor.

Taarifa pia zilisema mwili wa mwanadada huyo ulitolewa kwa familia yake na kusafirishwa hadi mochari ya Kiharu karibu na nyumbani kwao Gachie.

Inasemekana Ngumbu na Msando waliburudika pamoja kwa vinywaji Ijumaa jioni kabla baadaye kuviziwa na kisha kuuawa na watu wasiojulikana.

Miili yao ilipatikana Jumamosi asubuhi katika msitu wa Muguga mjini Kikuyu, Kaunti ya Kiambu.

Uchunguzi wa mauaji hayo unaendelea huku polisi wakisema, kufikia jana watu sita walikuwa wameandikisha taarifa kumhusu Msando.

Makachero wanawasaka watu wengine wanne akiwemo mwanamke ambaye picha za CCTV barabarani zilimnasa akiwa ndani ya gari la Msando kabla ya meneja huyo kutoweka.

Upasuaji maiti ya Ngumbu ulifanyika jana, siku moja baada ya upasuaji wa maiti ya Msando kufanywa Jumatano alasiri katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Lee mjini Nairobi.

Ripoti ya upasuaji ilisema Msando pia alikufa kwa kunyongwa koo. Vile vile, alikuwa amekatakatwa kwenye mkono wa kulia.

MSANDO NA CAROL NGUMBU WALINYONGWA HADI KUFA - MPASUAJI MSANDO NA CAROL NGUMBU WALINYONGWA HADI KUFA - MPASUAJI Reviewed by KUSAGANEWS on August 03, 2017 Rating: 5

No comments: