KINARA wa NASA, Raila Odinga, Alhamisi aliwatetea machifu kote nchini kutokana na vitisho vya Rais Uhuru Kenyatta kwamba atawafuta kazi watakaopatikana wakiunga mkono mungano wa NASA.
Akiongea mjini Kisumu wakati wa mkutano wa mwisho kabla ya uchaguzi mkuu, Bw Odinga aliwashauri machifu wapuuze vitisho vya Rais Uhuru Kenyatta.
“Uhuru alionya machifu kwamba Jubilee itawafuta kazi. Ninataka kuwaambia machifu mkifutwa kazi na Jubilee hiyo itakuwa ni leseni ya kupandishwa cheo na NASA. Uhuru atawafuta kazi kesho, lakini mtarudishwa kazini Jumatano wiki ijayo,” akasema Bw Odinga.
Alisema hayo kutokana na matamashi ya Rais Kenyatta mnamo Jumatano, akiwa katika Kaunti ya Makueni, ambako aliwatishia machifu kwa madai kuwa wamekuwa wakifanyia kampeni muungano wa NASA.
Mgombea mwenza, Bw Kalonzo Musyoka, aliwataka machifu wasijali wala kukubali kutishwa na serikali ya Jubilee.
“Pikipiki wanazotumia ni mali ya umma, maafisa wa serikali msitishwe,” akasema Bw Musyoka na kuwataka wananchi wajitokeze kwa wingi Jumanne kupiga kura kwa lengo la kutafuta uongozi mpya.
Kwenye taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa kampeni, Bi Kathleen Openda, NASA ilimkashifu vikali Rais Kenyatta kwa kuwatisha machifu katika eneo la Ukambani kwa madai ya kuunga mkono muungano huo. Kwenye taarifa iliyotolewa jana na afisa mkuu wa mawasiliano wa muungano huo, Bi Kathleen Openda, NASA ilisema matamshi ya Rais yanaonyesha Kenya kama nchi ambayo ingali inaongozwa kwa mfumo wa kidikteta.
“Kuwatishia machifu ni sawa na kuirejesha nchi katika mfumo wa kiimla. Rais anafaa kufahamu kuwa mambo yamebadilika, si kama ilivyokuwa zamani ambapo rais alikuwa anafanya maamuzi bila kuwajibika kwa yeyote,” ukasema muungano huo.
Wakati huo huo, alitangaza kuwa muungano wa NASA umebadilisha mikakati katika juhudi za kuhakikisha kuwa wafuasi wote wamepiga kura Agosti 8.
Bw Musyoka aliwashauri wananchi waondoke katika vituo vya kupigia kura baada ya kupiga kura zao na kwamba mabadiliko hayo yanalenga kuzuia vurugu katika vituo vya kupigia kura, hali yenye uwezo wa kuwahofisha wananchi wasipige kura.
“Baada ya kupiga kura, tunawashauri vijana waende kwenye maduka na kunywa chai na kungoja mpaka wakati wa kuhesabu kura,” akasema Bw Musyoka.
Alisema wananchi hawatawapa nafasi maafisa wa usalama kuwashambulia kwa vitoa machozi.
Hata hivyo, aliwataka maajenti wa Adopt a Polling Centre wawe makini madukani ili kuhakikisha kuwa watu wote waliojiandikisha kupiga kura wametekeleza haki yao ya kidemokrasia.
“Mpango wao ni kupiga watu ili wazue kutoelewana na kuzuia watu kupiga kura,” akasema Bw Musyoka.
Kwa upande wake, Bw Wetangula alisema, “Msimpe Matiang’i sababu yoyote ya kutekeleza mpango wake mwovu.”
Viongozi hao pia waliitaka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC) ihakikishe kuwa mfumo wa kielektroniki utakaotumiwa kupeperusha matokeo ya uchaguzi haukwami.
“IEBC ilifanyia mfumo huo majaribio Jumatano. Tunataka kuhakikishiwa kuwa hautafeli kwa sababu Wakenya hawatakubali iwapo mitambo hiyo haitafanya kazi,” akasema Bw Musyoka na kuungwa mkono na vinara wenza wa NASA.

No comments:
Post a Comment