WATU takribani 20 jana walijitokeza
kuuaga mwili wa anayedaiwa kuwa mbunifu wa nembo ya Taifa ya bibi na bwana,
Francis Maige maarufu Ngosha, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako
alikuwa akipatiwa matibabu kabla ya mauti kumfika Mei 29, mwaka huu.
Miongoni mwa watu waliojitokeza
kuuaga mwili huo, ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Global Publishers, Erick Shigongo
na mchoraji maarufu wa vibonzo, Nathan Mpangala.
Wengine ni Mkurugenzi wa Baraza la
Sanaa la Taifa (Basata), Godfrey Mngereza, Rais wa Shirikisho la Sanaa za
Ufundi (Tafca), Adrian Nyangamalle na Msajili wa Taasisi zisizo za kiserikali
(NGO's) wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wazee na Watoto, Marcel
Katemba.
Akizungumza wakati wa kuuaga mwili
huo, Mkurugenzi wa Huduma za Dharura wa Muhimbili, Dk. Juma Mfinanga, alisema
uchunguzi ulibaini kwamba alikuwa akiugua kifua kikuu (TB).
“Inaonesha TB hiyo alikuwa nayo kwa
muda mrefu na kwa kuwa alichelewa hospitalini, ilikuwa imekula mno ndani ya
mwili wake, alikuwa na maumivu ya kifua, tulijitahidi kuokoa maisha yake lakini
haikuwezekana,” alisema.
Alisema mzee huyo alikuwa na miaka
86 na kwamba alikosa lishe na malezi bora.
“Kitaalamu mzee akikosa lishe
inayotakiwa na malezi bora, ni rahisi kupata magonjwa mengi nyemelezi ikiwamo
TB, ni vema watu wakajenga tabia ya kupima afya zao na wazee wapewe malezi
bora,” alisema.
Kutokana na kuibuka utata wa nani
hasa ni mchoraji wa nembo ya Taifa, akizungumza katika shughuli ya kuaga mwili
wa Ngosha, Mkurugenzi wa Basata, Mngereza, alisema kuanzia sasa Serikali
itahakikisha wasanii wote wanafuata utaratibu ili watambulike na kazi zao.
“Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, ameniagiza pia kukabidhi ubani wa Sh
300,000 ambazo atakabidhiwa muuguzi anayeondoka na msafara kwenda Mwanza
akazifikishe kwa familia ya marehemu,” alisema.
Naye mchora vibonzo Mpangala alisema
wakati umefika kwa Serikali kufanya utafiti wa kutosha kupata taarifa sahihi za
watu waliosaidia Taifa kwa kubuni na kuchora vitu mbalimbali.
WATU 20 PEKEE WAJITOKEZA KUUAGA MWILI WA MCHORAJI NEMBO YA TAIFA YA BIBI NA BWANA
Reviewed by KUSAGANEWS
on
June 04, 2017
Rating:

No comments:
Post a Comment