Serikali ya Tanzania imepiga marufuku vituo vya Umma
kuwalipisha wananchi wanaokwenda kupima maambukizi ya ugonjwa wa Malaria kwa
kipimo cha MRDT na utoaji wa dawa za mseto (ALUU) zinazotumika kutibu ugonjwa
huo kuanzia sasa.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kilele cha
maadhimisho ya siku ya Malaria duniani mjini Dodoma, Waziri wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Bi. Ummy Mwalimu amesema vipimo hivyo ni bure
na pia mgonjwa asilipishwe fedha kwa dawa za mseto.
“Napenda kusisitiza vituo vya umma vinavyotumia vipimo vya
MRDT kwa wagonjwa wa malaria, vipimo hivyo ni bure na pia mgonjwa asilipishwe
fedha kwa dawa za mseto ama yule anayelazwa kuchomwa sindano ya ugonjwa
huo….Waganga wakuu wa mikoa na wilaya, hakikisheni kuanzia sasa mnafuatilia
wahudumu wote na watakaokiuka agizo hili watachukuliwa hatua za kisheria mara
moja”. Alisema Bi. Ummy
Aidha, Bi. Ummy amewataka wananchi kushirikiana na serikali
kuwafichua wahudumu wa Afya ambao watawalipisha fedha pindi watakapo kuwa
wanapima huduma ya Malaria kupitia kipimo cha MRDT ama watakapohitajika kupewa
dawa ya mseto (ALUU), pia amezionya maabara binafsi ambazo zimekuwa
zikifanya kazi zake kwa kuangalia zaidi fedha badala ya maisha ya mtu kama
kuwaambia wana maambukizi ya malaria wakati hawana.
Pamoja na hayo, amesema takwimu kutoka katika vituo vinavyotolea
huduma za afya zinaonyesha takribani watu milioni 12 wanaugua ugonjwa huo kwa
mwaka ambapo katika tafiti hizo mkoa wa Kagera, Geita na Kigoma ziliweza
kuonekana na viwango vikubwa vya maambukizo kwa mwaka 2015 na 2016 huku
wajawazito na watoto chini ya miaka mitano kuonekana kuathiriwa zaidi.
Waziri wa Afya ataja vipimo na dawa za malaria zinazotakiwa kutolewa bure
Reviewed by KUSAGANEWS
on
April 25, 2017
Rating:
Reviewed by KUSAGANEWS
on
April 25, 2017
Rating:


No comments:
Post a Comment