MBUNGE wa
Ngorongoro, Emmanuel Ole Shangai ameitaka serikali kuja na kauli moja inayotaka
wakazi wote wa eneo la Ngorongoro kuondoka kwa lazima kuliko kuendelea kufanya
alichokiita kuwawekea vikwazo katika huduma muhimu za kijamii, ikiwamo
upatikanaji maji safi na salama.
Shangai alitoa kauli hiyo bungeni wakati akichangia mapatio na
mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya
Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa mwaka ujao wa fedha.
Amesema kuwa kwa sasa hali ya wakazi wa eneo la Ngorongoro
imeendelea kuwa ngumu kutokana na vikwazo wanavyowekewa.
Mbunge huyo amesema serikali inatakiwa itoe tamko kwa wananchi
zaidi ya 108,000 walioamua kubaki katika Tarafa ya Ngorongoro baada ya wale
wengine 7,000 kuhamia Msovera na wao watoke kwa lazima kwa kuwa huduma nyingi
zimefungwa kwa sasa.
Ametaja huduma zilizofungwa kwa wananchi hao kuwa ni pamoja na
zaidi ya shule 27 za msingi katika tarafa hiyo ambazo aliliambia Bunge kuwa
zote zimezuwa kujenga wala kukarabati vyoo, hali inayosababisha walimu na
wanafunzi kujisaidia porini.
Mbunge huyo pia amesema kuna shule ya msingi ya bweni
imesitishiwa huduma ya maji, hali inayowalazimu wananchi kufuata huduma ya maji
mtoni na kuhatarisha maisha yao.
“Kwanini tunafanya hivi? Kila mwananchi ana haki ya kupata
huduma na zoezi la kuhama lilikuwa la hiari na Waziri Mkuu alipozungumza na
wananchi alithibitisha hilo. Iweje sasa tuanze kuwawekea vikwazo vya
maendeleo?" Shangai amehoji.
Amesema ni zaidi ya miaka mitatu sasa wananchi hawapati huduma
stahiki zikiwamo huduma za afya ambazo zimekuwa hafifu na kuhoji wananchi
wameikosea nini serikali kwa kuwa wako katika eneo hilo kisheria.
Mbunge huyo amesema licha ya jimbo kupata maendeleo mbalimbali
ikiwamo kujengwa shule za sekondari na msingi kutokana na jiografia ya
mazingira ya wanyama katika shule hizo, wanafunzi hawatafaidi kutokana kutokuwa
na mabweni pamoja na nyumba za walimu ili wanafunzi wapate huduma ipasavyo.
“Wakati wa hotuba ya kuhitimisha hoja hii, mniambie kwamba
serikali ina mpango gani na wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro?
Isitoshe kwenye geti la Ngorongoro wananchi wakirudi jioni
hawaruhusiwi kuingia mpaka wawe na vitambulisho vya wapigakura ilhali wapo
baadhi ya vijana wenye umri wa chini ambao wanawalazimisha kwenda polisi
kuchukua taarifa inayowatambulisha,” amesema.
Mbunge Shangai pia amesema hata wafanyabiashara wa mifugo
wanazuiwa kufanya shughuli zao, wakitakiwa kubeba ng’ombe kwa malori ilhali
hakuna miundombinu ya barabara ya kupitisha magari hayo.
“Kama imefika wakati ni bora tuwaambie kwamba hawahitajiki
katika eneo hilo ili waondoke kuliko kuendelea kuwapa mateso maana upo pia
mradi wa elimu wa wanafunzi kusomeshwa vyuo vikuu na vyuo vya kati, lakini
wanafunzi zaidi ya 154 waliopitishwa na Baraza la Wafugaji wamesitishiwa
ufadhili hali inayosababisha ongezeko la watoto wa kike kujihusisha na vitendo
vibaya vya kujiuza ili kupata chochote,” amesema.
Vilevile, amesema wafanyabiashara wameanza kugomea minada baada
ya serikali kupitia halmashauri kuongeza kodi katika mifugo ambapo kwa mbuzi
imeongezeka kutoka Sh. 2,500 hadi 8,000 huku madiwani, Mwenyekiti wa
Halmashauri wakiwa hawajui na ushuru huo unakusanywa kwa kutumia wanajeshi.
Katika hotuba yake bungeni wiki iliyopita wakati wa kuwasilisha
hoja hiyo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa atika jitihada za kulinda
bioanuai ya hifadhi na kuboresha maisha ya wananchi wanaoishi ndani ya Hifadhi
ya Ngorongoro, serikali imeendelea kuwahamisha kwa hiari wananchi kutoka ndani
ya eneo la hifadhi kwenda katika maeneo yaliyotengwa na serikali huko Msomero
wilayani Handeni, Saunyi (Kilindi), Kitwai (Simanjiro) na maeneo mengine ambayo
wananchi wamechagua.
Waziri Mkuu amesema kuwa katika awamu ya pili, jumla ya nyumba
5,000 zinajengwa katika maeneo ya Msomera (2,500), Saunyi (1,000) na Kitwai
(1,500) ambapo katika kipindi cha kuanzia Julai 2023 hadi 21 Februari 2024,
jumla ya nyumba 700 zimekamilika na nyumba 1,800 ziko katika hatua mbalimbali
za ujenzi.
"Katika kipindi cha Julai 2023 hadi Februari 2024, jumla ya
kaya 491 zenye watu 3,451 na mifugo 14,599, zimehama kwa hiari na hivyo kufanya
jumla ya kaya zilizohamia tangu kuanza kwa zoezi hili Julai 2022 kufikia 1,042,
ikijumuisha jumla ya watu 6,461 na mifugo 29,919," Majaliwa amefafanua.
No comments:
Post a Comment