WANDISHI WA HABARI WAPATA MAFUNZO MAALUM KUTOKA MAMLAKA YA HIFADHI NGORONGORO

Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) imewanoa waandishi wa habari mkoa wa Arusha kuhusiana na umuhimu wa urithi wa kitamaduni unaopatikana katika hifadhi hiyo ikiwemo ushahidi wa kipekee unaoelezea ni lini binadamu alianza kutembea kwa miguu miwili.

Akiongea na waandishi wa habari katika semina hiyo kamishna msaidizi mwandamizi idara ya urithi wa utamaduni na jiolojia, Muhandisi Joshua Mwankunda alisema kuwa  uridhi wa kitamaduni ni muhimu hasa katika eneo la Olduvai ambako ndipo kuna taarifa za chimbuko la mwanadamu lakini pia eneo la Laetole ambako ndipo zilipo nyayo za Zamadam.

Muhandisi  Mwankunda alisema kuwa Nyayo za Zamadam wa Laetole zilipatikana takribani miaka milioni 3.5 mpaka milioni 3.7 ambapo umuhimu wake ni kuelezea binadamu walipotoka.

Alieleza kuwa katika blonde la Olduvai  kilichopatikana pale kinaunganika na kilichopatikana eneo la Laetole na kuelezea kwa ujumla wake mwendelezo mpaka leo kuhusiana na chimbuko la mwanadamu na mabadiko yake katika kuishi na kupambana na mazingira yake.

“Vitu vya muhimu ambavyo tumeongelea Leo ni umuhimu na upekee wa hizi rasilimali kwasababu zipo maeneo mengine Duniani lakini kwa Tanzania Nyayo za Zamadam wa Laetole ni ushahidi pekee katika mfumo wa kuthibitisha ni lini sisi wanadamu tulianza kutembea kwa miguu miwili katika hii miaka milioni 3.5 ambapo hakuna ushahidi wa namna hii tena maeneo mengine kwani inawezekana ushahidi wa Zamadam wale, kwa umri ule na kwa maumbile yale lakini ushahidi wa kwamba walitembea kwa miguu miwili upo Laetole peke yake,”Alisema.

Alifafanua kuwa baada ya ugunduzi ule, gunduzi zingine zozote za viumbe wa aina Ile zinakuwa zinaelekezwa katika eneo hilo ambapo inanifanya Tanzania kuwa katika ramani ya kidunia katika kupata taarifa za kisayansi kuhusiana na chimbuko la mwanadamu.

“Katika bonde la Olduvai tumeelezea uwepo wa yale makundi mengine matatu Homo habilis, Homo erectus na Homo sapiens ambaye baadae tulikuja kuwa sisi ambapo tumeona masalia yale ya kibaolojia yamepatikana katika bonde like sambamba na masalia yanayothibitisha mabadiliko ya tabia Kwa mfano matumizi ya dhana za  mawe katika hatua mbalimbali, teknolojia na stadi pamoja na tabia za namna wale Zamadam walivyoishi katika eneo hilo,” Alieleza.

“Olduvai ni eneo pekee ambalo Duniani masalia yake yamehifadhika katika ubora wa hali ya juu na zinapofanyika tafiti yanapatikana katika ubora lakini muunganiko wa makundi yote yapo sehemu moja tofauti na maeneo mengine Duniani,”

Kuhusiana na eneo la watafiti wa zamani(Leakey Camp) Kamishna huyo alisema kuwa  eneo hilo limefanyika kuwa makumbusho kwani ni kambi ya kwanza Africa ya watafiti ambapo kutokana na wao kuwepo eneo hilo kuliwezesha kufanya gunduzi ambazo zilileta hamasa kwa watafiti wengine Duniani kuja katika eneo lile na kuchangia kugundua vitu vingine ambavyo wamevielezea.

“Awali ilikuwa inafikirika pengine labda chimbuko la binadamu wa kwanza liko Asia lakini baada ya watafiti wale kukaa pale na kugundua lile fuvu linaloitwa  ilieta hamasa na uelewa kwa Dunia nzima ambapo katika Kambi Ile ambayo sasa  ni makumbusho utaona jinsi watafiti wale walivyoishi, vifaa walivyovitinia, njia walizozitumia kuishi katika mazingira ambayo kwa wakati huu yalikuwa ni magumu lakini waliweza kufanya gunduzi hizi za muhimu,”Alisema.

Kwa upande wake mkuu wa wa kitengo cha habari katika mamlaka hiyo  Joyce Mgaya alisema kuwa alisema kuwa Lengo la semina hiyo ni kuelezea waandishi wa habari umuhimu wa eneo la hifadhi ya Ngorongoro ili kuhakikisha kile ambacho kipo katika hilo kinafahamika kwa umma kwani wanatambua kuwa kupitia kazi za waandishi na kalamu zao  wananchi wanapata kuelimika na kuhabarishwa.

 

WANDISHI WA HABARI WAPATA MAFUNZO MAALUM KUTOKA MAMLAKA YA HIFADHI NGORONGORO WANDISHI WA HABARI WAPATA MAFUNZO MAALUM KUTOKA MAMLAKA YA HIFADHI NGORONGORO Reviewed by KUSAGANEWS on February 10, 2022 Rating: 5

No comments: