MAMA ASIMULIA MWANAWE ALIVYOTAKA KUMUUA


Mama mzazi wa mtoto wa miaka 15, Anastasia Dastani amesimulia jinsi mwanawe alivyojiingiza kwenye uhalifu hatimaye mtoto huyo kufanya jaribio la kutaka kumuua kwa kumuwekea sumu kwenye mboga.

Mtoto huyo ambaye alikuwa anasoma darasa la sita katika Shule ya Msingi Buyuni, wilayani Ilala, Dar es Salaam, amekamatwa juzi na askari wa ulinzi na usalama wa Taasisi ya TPSIS, akiwa na wenzake wanaodaiwa kuwa ni mafundi wa luninga eneo la Kwazoo.

Wenzake hao ni pamoja na Herman Kiwale na Miraji Alex, wanaodaiwa kuiba luninga, deki na fedha taslimu Sh200,000 mali ya mkazi wa Zavala, Sauda Isakile.

Anastazia alisema mwanawe alianza tabia ya wizi tangu mwaka 2019, hali iliyomfanya ashindwe kuhudhuria masomo na hatimaye alifukuzwa shule.

“Mwanangu tabia ya wizi anayo, huu ni mwaka wa tatu, huwa anarudi nyumbani usiku wa kuanzia saa 5 na ninapomuuliza ametoka wapi huwa ananijibu niachane naye,” alisimulia Anastazia jana, alipokuwa Ofisi ya Kata ya Buyuni zilipo ofisi za TPSIS baada ya mwanawe huyo kukamatwa.

Alisema huyo ni mtoto wake wa tano na anapoenda kuiba, wenzake humpitisha dirishani, wao hubaki nje na kupokea mali zinazoibwa ndani.


Anastazia alisema tabia ya wizi wa mtoto wake alikuwa haipendi na kila alipomkanya alikuwa akimtolea lugha chafu.

“Siku moja nilimuonya kuhusiana na wizi huo, baadaye aliondoka na kuelekea Gongolamboto, aliporudi alipika ugali ili ale na mjukuu wangu, sasa nilipokata tonge la ugali na kuchovya kwenye mboga kisha kupeleka mdomoni, nilisikia harufu kali ya sumu ya panya.

“Nilipomuuliza mtoto wangu hii mboga ni ile niliyopika au kuna nyingine, alinijibu achana na mimi, nikaimwaga, niliporudi ndani akaniambia una bahati nilitaka ufe kama alivyokufa baba yangu. Niliweka sumu. Aliposema hivyo nilienda kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wakamkamata na kumpeleka kituo cha polisi cha Stakishari,” alisema Anastazia.

Alisema walipomhoji alidai alipewa sumu hiyo na mtu aliyemtaja kwa jina la Chito.

Mtoto ahojiwa

Alipohojiwa na askari wa TPSIS alikiri kuwa wizi alifundishwa na mtu aliyemtaja kwa jina moja la Kiwale.

Alisimulia kuwa wanapoenda kuiba kwenye nyumba mbalimbali, yeye huingia ndani kwa kupitia dirishani, huku fundi huyo akimpokea vitu mbalimbali walivyoiba, zikiwamo luninga na deki.

Alisema hufanya matukio hayo nyakati za usiku na mchana. “Tukifika kwenye nyumba Kiwale anakata nondo za madirisha halafu ananipitisha kwenye dirisha.

“Jana tulienda Zavala muda wa mchana na tulipofika kwenye nyumba, mimi nilijaribu kuvunja kioo cha dirisha nikashindwa, ndipo fundi akavunja na kukata nondo nikaingia ndani, yeye akabaki nje na kunipokea luninga na deki nilizoiba, vitu hivi huwa tunaenda navyo ofisini kwake,” alisema mtoto huyo.

Alisema kabla hawajaenda kufanya tukio Kiwale huwa anamtuma afuatilie nyumba ambazo zina luninga, redio zenye sabufa, deki na fedha taslimu na akishampelekea taarifa wanaenda kuiba.

Mtoto huyo alidai kuwa wakishaiba vitu mbalimbali na kuvipeleka kwenye ofisi ya fundi huyo huwa anamlipa kiasi cha Sh2,000 hadi 3,000 na anapokataa kwenda kuiba huwa anatishiwa kuuawa na Kiwale.

Alisema anashirikiana na watoto wenzake akisema mmoja ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi Buyuni.

Mtoto huyo aliyataja maeneo ambayo wamefanya uhalifu huo katika kata ya Buyuni ni eneo la Zavala, Chepa, Kigezi na Mbiki.

Askari wa ulinzi na usalama Kata ya Buyuni, Shabani Mtatura alisema alipewa taarifa na watu walioibiwa vitu hivyo, ndipo walifuatilia na kubaini mtoto huyo alishirikiana na mafundi wa luninga kuiba vitu hivyo pamoja fedha taslimu Sh 200,000.

“Tuliwakamata watuhumiwa hao na kutoa taarifa kwa Mkuu wa kituo cha Polisi Chanika wakaja kwenye kata hii na kuwachukua kwa ajili ya hatua za kisheria zaidi,” alisema Mtatura.

Mtatura alisema katika operesheni hiyo wamemkamata mtuhumiwa Adeus Antoni akiwa na kete 53 na bangi.

MAMA ASIMULIA MWANAWE ALIVYOTAKA KUMUUA MAMA ASIMULIA MWANAWE ALIVYOTAKA KUMUUA Reviewed by KUSAGANEWS on July 18, 2021 Rating: 5

No comments: