Zaidi ya biashara 140 zimefungwa mkoani hapa katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Januari mpaka Machi 31, mwaka huu kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo madeni kwa wafanyabiashara.
Hayo yalibainishwa
juzi na Meneja Msaidizi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Njombe,
George Mapunda kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa (RCC) kilichofanyika
mjini hapa.
Alisema
wafanyabiashara wengi wamekuwa na uelewa mdogo kuhusu masuala ya kodi, licha ya
mamlaka hiyo kuwa na kitengo cha kutoa elimu kwa mlipa kodi na wamekuwa
wakipita maeneo mbalimbali kutoa elimu hiyo.
“Kuna timu kutoka
makao makuu na ile ya hapa walipita mlango kwa mlango ili kuelimisha wananchi.
Walikwenda Ludewa, Makambako na Njombe mjini na sisi ratiba ya kuwatembelea
wadau wetu ipo palepale,” alisema Mapunda.
Alisema
wafanyabiashara wadogo wanatozwa kodi kulingana na kumbukumbu ya mauzo ambayo
ipo kisheria, hivyo wanapouza na kutumia mashine wanaweza kutambua kiasi cha
kodi wanachostahili kulipa pasipo kusumbuliwa.
Hata hivyo, alisema
kama mfanybiashara hajaridhishwa na makadirio ya kodi aliyopatiwa anapaswa
kwenda ngazi za juu na tatizo hilo likatatuliwa.
ADVERTISEMENT
“TRA haifungi biashara
ya mtu, kuna watu wanadaiwa lakini hatufungi biashara, tunachofanya tunakuita
tunakaa mezani tunakwambia ulipe na deni lako ni hili kisha tunaingia katika
makubaliano ya kulipa kwa awamu,” alisema Mapunda.
Alitoa rai kwa
wafanyabiashara kutunza kumbukumbu za mauzo ili kukadiriwa kiasi cha kodi
kulingana na mauzo.
Mkuu wa Mkoa wa
Njombe, Mhandisi Marwa Rubirya aliitaka TRA mkoani hapa kuzingatia maelekezo
yaliyotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwataka kukusanya kodi kwa weledi
na kuacha kutumia mbinu zinazoua biashara.
Alisema mamlaka hiyo
ina wajibu wa kisheria wa kuhakikisha wanahamasisha ukusanyaji wa kodi kutoka
kwa wafanyabiashara kwa hiari pasipo kutumia mabavu na kwamba, elimu
inayotolewa inapaswa kuendelea ili kujenga ufahamu.
No comments:
Post a Comment