Chama cha ACT-Wazalendo kimesema kinajipa muda zaidi wa kutafakari iwapo itapendekeza jina la makamu wa kwanza wa rais wa Zanzibar pamoja na kushiriki katika Serikali ya Umoja ya Kitaifa (SUK).
Kauli hiyo ilitolewa jana na
Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad wakati akizungumza na
gazeti hili lililotaka kujua msimamo wa chama hicho kuhusu ushiriki wake katika
SUK, kutokana na msimamo wake wa awali kutotambua Uchaguzi Mkuu uliopita na
matokeo yake.
Kwa mujibu wa Ibara ya 39 ya Katiba
ya Zanzibar ya mwaka 2010, Rais wa Zanzibar atamteua Makamu wa Kwanza wa Rais
mwenye sifa za kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na atateuliwa na Rais baada
ya kushauriana na chama kilichotokea nafasi ya pili katika matokeo ya kura ya
Uchaguzi wa Rais.
Hata hivyo, chama kilichotokea
nafasi ya pili katika uchaguzi kinatakiwa kiwe kimepata si chini ya asilimia 10
ya kura zote.
Katika matokeo ya urais Zanzibar
yaliyotangazwa Oktoba 29, mwaka huu Maalim Seif aliyegombea urais kupitia ACT
alipata asilimia 19.87.
Kwa mujibu wa Katiba hiyo ya
Zanzibar, pamoja na uteuzi huo na Rais atafanya mashauriano kuhusu uteuzi wa
mawaziri kutoka upinzani.
Advertisement
Kulingana na katiba hiyo iliyotokana
na maridhiano ya mwaka 2010 yaliyofanyika baina ya Rais wa sita Amani Abeid
Karume na Maalim Seif, makamu wa kwanza wa Rais atakuwa ni mshauri mkuu wa Rais
katika kutekeleza kazi zake na atafanya kazi zote atakazopangiwa na Rais.
Ndani ya siku saba zinazotajwa na
Katiba, Dk Mwinyi amemteua Hemed Suleiman Abdulla kuwa mjumbe wa Baraza la
Wawakilishi na kisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Baada ya muda huo kupita na kimya
kutawala kuhusu nafasi ya makamu wa kwanza wa Rais, Mwananchi lilimtafuta
mwenyekiti huyo wa ambaye alisema bado kuna muda kwa kuwa Katiba ya Zanzibar
inatoa siku 90 kwa chama kitakachotoa makamu wa kwanza wa rais kupeleka jina
ikiwa hakikuweza kufanya hivyo katika siku saba za mwanzo.
“Kamati kuu (ya ACT Wazalendo)
iliamua tusikimbilie katika siku saba kwa sababu kuna mambo yanayohitaji
tafakuri ya kina. Pia katika jambo kubwa kama hili na mazingira ya huu unaoitwa
uchaguzi ni vizuri kuwashirikisha wanachama wenzetu katika kutoa ushauri wao
kwa kuwa ndio waathirika,” alisema Maalim Seif.
Alipoulizwa watawashirikishaje
wanachama hao, Maalim Seif ambaye aliwahi kuwa makamu wa kwanza wa Rais
Zanzibar alisema “kuwashirikisha wanachama wetu sio jambo geni. Tunafanya vikao
vya ndani na wanachama katika maeneo mbalimbali ya Unguja na Pemba na kuwaomba
watoe maoni yao kwa uhuru.”
Maalim Seif ambaye pia aliwahi kuwa
Waziri Kiongozi wa Zanzibar alisisitiza kuwa ACT-Wazalendo imeamua kujipa muda
wa kutosha katika kufanya uamuzi wa suala hilo huku akisema kuhusu
ushirikishwaji wa wananchi chama kinajipanga pia.
Kwa nyakati tofauti Rais wa awamu ya
nane wa Zanzibar, Dk Mwinyi aliyepata kura 380,402 sawa na asilimia 76.27,
amesema ataendeleza maridhiano yaliyopo kikatiba pamoja na kudumisha amani
iliyopo kwa kushirikiana na wapinzani kwa kuwa ni nyenzo muhimu katika kukuza
demokrasia nchini.
No comments:
Post a Comment