Wajawazito 975 Kilimanjaro wakutwa na VVU


WAJAWAZITO 24,000 waliopimwa Virusi vya Ukimwi katika mkoa wa Kilimanjaro, 975 wamekutwa na maambukizi ya virusi hivyo ikiwa ni sawa na asilimia nne

Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Shirika la Elizabeth Glaser Pediatric Aids Foundation (EGPAF), Jacquesdol Massawe alisema wajawazito hao ni kati ya wananchi 168,825 waliofikiwa na huduma za upimaji na ushauri nasaha katika vituo vinavyofikiwa moja kwa moja na mradi wa USAID Boresha Afya

Massawe alikuwa akizungumza jana katika Wilaya ya Mwanga, wakati wa mkutano wa wadau wa VVU na Ukimwi mkoani Kilimanjaro ambao uliongozwa na Mkuu wa mkoa huo, Anna Mghwira

“Ukiachilia mbali hao akina mama wajawazito, kuna watu wengine 4,953 nao walipatikana na maambukizi ya VVU ikiwa ni sawa na asilimia 2.9 lakini pia wananchi 4,338 wameanzishiwa dawa za kufubaza makali ya virusi vya ukimwi,”alisema

Alisema wananchi hao walifanyiwa vipimo hivyo, kati ya Aprili mwaka 2017 hadi Machi mwaka huu na kwamba mradi wa USAID Boresha Afya na kamati ya afya ya mkoa na halmashauri saba za mkoa wa Kilimanjaro zimewezesha asilimia 98 ya wananchi wote wanaopata huduma za tiba na matunzo kufanyiwa uchunguzi wa kifua kikuu na waliopatikana na dalili wamepatiwa huduma stahiki

Mradi huo unaboresha huduma za kinga na matibabu ya virusi vya ukimwi na ukimwi, uzazi wa mpango na kifua kikuu kwa ufadhili wa Mpango wa Rais wa Marekani wa kupambana na VVU (PEPFAR), kupitia Shirika la Maendeleo la Watu wa Marekani (USAID

Aidha, kupitia mradi huo halmashauri saba za mkoa wa Kilimanjaro, kamati ya afya ya mkoa na Hospitali ya Rufani ya KCMC zimetengewa kiasi cha Sh. Bilioni 1.5 ili kutekeleza afua za upimaji na matibabu

Awali, Mganga Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Dk. Best Magoma akizungumza na wadau hao alisema mkutano huo unalenga kuunga mkono kampeni ya ‘Pima, Jitambue, Ishi’ iliyozinduliwa hivi karibuni na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

“Humu wote tumekuja kushirikishana uzoefu na mafanikio ya mipango ya kimkakati na hatimaye kujadili changamoto na namna ya kuzitatua ili kufikia malengo mahususi ya 90-90-90 ifikapo mwaka 2020,”alisisitiza Dk. Magoma

Akifungua mkutano huo, Mkuu wa mkoa huo, alisema kuna kila sababu ya kufanya vizuri kutokana na serikali ya Rais John Magufuli kufanikiwa kuviunganisha vituo vyote vya afya vya umma na vituo vya afya na hospitali zinazomilikiwa na sekta binafsi

“Unajua huko nyuma tulitoa vitu karibu vyote kwenye mikono ya umma na tukaacha jukumu hilo kutekelezwa na sekta binafsi lakini sasa tunataka kwenda mbele. Kwa hiyo ni lazima tuanze ku-reverse (kurudi) na kuimarisha huduma za umma,”alisisitiza Mghwira
Wajawazito 975 Kilimanjaro wakutwa na VVU Wajawazito 975 Kilimanjaro wakutwa na VVU Reviewed by KUSAGANEWS on July 21, 2018 Rating: 5

No comments: