Mtu
mmoja kati ya wanne waliokamatwa katika operesheni ya kudhibiti uvuvi
haramu Ziwa Victoria, amefariki dunia kutokana na kile kinachodaiwa kuwa
alipata kipigo kutoka kwa askari wanaosimamia operesheni hiyo.
Aliyefariki dunia ni Paschal Kanyembe (40), mkazi wa Kitongoji cha Mlila, Kijiji cha Rubambangwe wilayani Chato mkoani Geita.
Mbali
na Kanyembe, watuhumiwa wengine waliokamatwa na kudaiwa kujeruhiwa
katika operesheni hiyo ni Busu James, Emmanuel Luchagula na Rusato
Magesa.
Akizungumzia
tukio hilo, mke wa marehemu, Ester Justine (39), alisema juzi kuwa
majira ya saa saba usiku wa kuamkia Jumanne, askari wa doria ya
kudhibiti uvuvi haramu walifika nyumbani kwake na kutoa amri kwa
wanandoa hao kufungua mlango.
Alisema
walilazimika kuomba dakika chache ili wavae na askari hao walikubali na
kuwapatia dakika mbili za kufanya hivyo na baadaye wanandoa hao
walifungua mlango wa nyumba yao.
Ester
aliendelea kueleza kuwa, pasi na kujua kinachoendelea, askari wawili
kati ya kundi kubwa lililokuwa nyumbani kwake, waliingia ndani na
kumweka chini ya ulinzi mume wake huku wakimtaka kusalimisha nyavu
haramu walizodai amezificha.
"Baada
ya mume wangu kuwaambia kuwa hausiki na uvuvi wa aina yoyote ile,
walianza kumshambulia kwa marungu na mateke huku wakimvuta kwenda nje,"
Ester alieleza.
"Hata walipomfikisha nje waliendelea kumpiga sana hadi akashindwa hata kukaa chini, akabaki amelala chali.
"Nikiwa
mlangoni, nilishuhudia kipigo hicho, lakini baadaye askari waliniamuru
kurudi ndani kulala huku wakiondoka na mume pamoja na vijana wengine
watatu ambao tayari walikuwa wameshawekwa chini ya ulinzi.
"Majira
ya saa mbili asubuhi leo (Jumanne) nilipiga simu ya mume wangu ili
kujua kama ameachiwa lakini ilipokelewa na mmoja wa askari hao ambaye
alianza kuniuliza kama mume wangu huwa ana ugonjwa wa kifafa, kisukari
au shinikizo la damu.
"Nilipowajibu
kuwa hajawahi kuugua magonjwa hayo, wakaniambia 'tafuta usafiri uje kwa
mume wako yupo huku Kituo cha Afya cha Nyabugera Muganza'. Ikabidi
niende huko."
Ester
aliongeza kuwa mume wake alipelekwa katika kituo hicho na askari
hao.Rafiki wa marehemu, Didas Emmanuel, alisema juzi kuwa baada ya
kufika Kituo cha Afya Muganza akiwa na Ester, alishuhudia rafiki yake
akiwa hajiwezi huku akiwa anaongezwa maji mwilini kwa sindano.
Alisema
kuwa matabibu waliokuwa wanampa kituoni hapo, walimshauri kwenda kituo
cha polisi kuchukua fomu ya polisi ya kuruhusu mtu aliyejeruhiwa
kutibiwa (PF3) kabla ya mgonjwa wao kuhamishiwa Hospitali ya Wilaya ya
Chato kwa ajili ya matibabu zaidi.
"Tukiwa
njiani kwenda hospitali ya wilaya kumwahisha mgonjwa wetu ili apatiwe
matibabu, majira ya saa 5:30 asubuhi, ndugu yetu alikata roho," alisema.
Wakazi
wengine wa eneo hilo, Daud Kingu na Enos Petro, walidai vitendo vya
askari wa doria ya uvuvi haramu kupiga wananchi ovyo, kuvamia nyumba za
watu usiku, kupora simu na fedha za wananchi vimekuwa vikitokea mara kwa
mara kwenye maeneo yao.
Mganga
Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Chato, Dk. Eligobeth Kalisa, alikiri
kupokea maiti ya mtu huyo pamoja na wagonjwa wengine watatu
waliopelekwa na Idara ya Maliasili ambao walitibiwa na baadhi yao
kuruhusiwa kuondoka baada ya afya zao kuimarika.
"Itoshe
tu kusema kuwa taarifa za uchunguzi (Kanyembe) tumeshawapatia polisi.
Na unajua mambo haya yakishakuwa kwenye jinai, sisi haturuhusiwi
kuyazungumzia. Kwa hiyo, mambo mengine watafute polisi," alisema Dk.
Kalisa.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo, alithibitisha kutokea kwa
tukio hilo na kudai kuwa kifo hicho kilitokea kwa bahati mbaya kwa kuwa
lengo la askari hao ni kudhibiti uvuvi haramu na siyo vingine.
"Ni
kweli tukio hilo lipo na umauti ulimkuta kijana huyo jana (juzi) majira
ya saa sita mchana akiwa amefikishwa kwenye Kijiji cha Mkuyuni wakati
akiwahishwa hospitali kwa matibabu zaidi baada ya kumpatia rufani kutoka
Kituo cha Afya cha Nyabugera. Kijana huyo alipungukiwa nguvu na umauti
kumkumba," alisema Mwabulambo.
Mwingine afia Mikononi mwa Polisi
Reviewed by KUSAGANEWS
on
July 25, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment