Mbunge wa zamani CUF ajiunga CCM


Mbunge wa zamani wa viti maalumu (CUF), Amina Mwidau amejivua uanachama wa chama hicho na kutangaza kujiunga na CCM

Amina katika taarifa aliyoisambaza kwenye vyombo vya habari jana, alisema sababu ya kuhama CUF ni kutaka kujipanga kivingine katika safari ya kuwaletea maendeleo wananchi

Alisema baada ya miaka miwili na nusu ya kutafakari mwenendo wa kisiasa ndani ya CUF na vyama vingine vya upinzani, pamoja na utendaji wa Serikali ya awamu ya tano ameamua kujivua uanachama wa chama hicho

“Nimeridhika sasa ni wakati muafaka wa kujipanga kivingine katika safari ya kushiriki kuleta maendeleo na ustawi wa wananchi wote,” alisema

Amina aliyekuwa mbunge mwaka 2010 hadi 2015 na aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), alisema ameamua kujiunga na CCM kwa sababu ana ndoto ya kuendelea kushirikiana na wananchi katika kuleta ustawi na maendeleo, hivyo hayupo tayari kuishia njiani.

Katibu wa CCM Mkoa wa Tanga, Allan Kingazi alisema kuwa Amina atapokewa rasmi na chama hicho kesho katika Uwanja wa Makorora Kati

Alisema mapokezi hayo yatafanyika sambamba na uzinduzi wa kampeni za udiwani katika Kata ya Makorora

Wakati huohuo, diwani wa Nasa (Chadema), Solomon Mmary amejiuzulu nafasi hiyo na kujiunga na CCM. Huyo ni diwani wa 51 wa Chadema kujiuzulu tangu mwaka 2015

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Siha, Valerian Juwal alithibitisha kupokea barua ya Mmary kujiuzulu, huku katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Jonathan Mabihya akieleza wamejipanga kumpokea na kumkabidhi kadi ya chama hicho leo

Mmary amejiuzulu siku chache tangu alipovuliwa uenyekiti wa Chadema wilayani Siha mkoani Kilimanjaro

Akizungumza na Mwananchi, Mmary alisema amechukua uamuzi huo ili kuunga mkono juhudi za kuleta maendeleo zinazofanywa na Serikali

Pia, alisema ni kutokana na vikwazo vilivyopo ndani ya chama alichohama ikiwa ni pamoja na kulalamikiwa kushirikiana na mbunge wa Siha (CCM), Dk Godwin Mollel ambaye awali alikuwa mbunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya Chadema

“Niligombea udiwani ili kushughulika na matatizo ya wananchi na baada ya kuchaguliwa niliamini siasa zimeisha, ni muda wa kufanya kazi hivyo nilifanya kazi ya kuleta maendeleo, lakini nimepata vikwazo vingi,” alisema
Mbunge wa zamani CUF ajiunga CCM Mbunge wa zamani CUF ajiunga CCM Reviewed by KUSAGANEWS on July 20, 2018 Rating: 5

No comments: