Udhalilishaji watoto St Florence wateka Bunge

Tukio la wanafunzi wanne wa kike wa darasa la saba katika Shule ya St Florence ya jijini Dar es Salaam kudaiwa kudhalilishwa kingono na mwalimu wao limeibukia bungeni baada ya wabunge kuitaka Serikali kueleza hatua zilizochukuliwa hadi sasa

Wabunge hao wa viti maalumu (CCM), Ester Mmasi na Zainabu Vulu wametoa kauli hiyo leo Alhamisi Mei 31, 2018 bungeni mjini Dodoma baada ya kipindi cha maswali na majibu.

Katika mwongozo aliouomba kwa kiti cha spika, Mmasi amesema moja ya mikataba ya kitaifa na kimataifa iliyoingiwa na Serikali ni kumlinda mtoto ili aweze kusoma na kufikia ndoto zake, lakini kwa sasa kumekuwa na kadhia ya kukosa ulinzi hususan mtoto wa kike.

“Katika mitandao ya kijamii kuna taharuku, wazazi wameripoti kuwa mwalimu Ayubu Mlumbu wa St Florence ya Dar es Salaam vitendo anavyowafanyia watoto wao, lakini mkuu wa shule alizuia taarifa zisifike serikalini,” amesema Mmasi

“Hapa ninapozungumza amewaathiri kisaikolojia watoto wanne. Lini Serikali itawalinda watoto?”

Kwa upande wake, Vulu amesema, “Nasimamia hapo hapo kwa Mmasi. Nina masikitiko na majonzi makubwa sana pamoja na wazazi wengine wanaume na wanawake. Nataka kujua ni nini Serikali itachukua  hatua. Wale bado ni watoto wadogo tena wa kike wameathirika kisaikolojia

Lakini picha zinasamba katika mitandao na sheria ipo inayowalinda watoto, Serikali inataka kutuambia nini kwa wale wanaosambaza picha mitandaoni na huyu aliyefanya hivi sheria inachukua hatua gani?”
Akitoa maelezo ya miongozo ya wabunge hao, mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge amesema miongozo hiyo inazungumzia matukio ambayo hayajatokea mapema leo, kama ambavyo kanuni za chombo hicho cha dola zinavyoeleza

“Lakini kwa vile ni tukio la kusikitisha, kufadhaisha na kuudhi na Serikali ipo na sheria za nchi zipo nadhani Serikali kama wataweza kulisemea hili nawapa fursa ya kufanya hivyo,” amesema Chenge

Akitoa ufafanuzi wa jambo hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama amesema, “Serikali imesikia kutoka kwa wabunge lakini kwa kweli hata sisi Serikali hili ni jambo linaloleta ukakasi.”

“Pamoja na ukakasi huu linahitaji kufanyia kazi ya kina, tunaomba tupewe nafasi ya kulifanyia kazi na kwa muda utakaoona inafaa Serikali ije iseme ndani ya Bunge.”

Udhalilishaji watoto St Florence wateka Bunge Udhalilishaji watoto St Florence wateka Bunge Reviewed by KUSAGANEWS on May 31, 2018 Rating: 5

No comments: