Rais Magufuli aishukuru Saudi Arabia kwa msa ada wa kujenga chuo kikuu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameishukuru Saudi Arabia kwa kutoa msaada wa kujenga chuo kikuu cha Kiislamu hapa nchini na ameahidi kuwa Serikali itatoa ushirikiano kufanikisha ujenzi wa chuo hicho

Mhe. Rais Magufuli ametoa shukrani hizo tarehe 28 Mei, 2018 Ikulu Jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kumaliza futari aliyowaandalia wageni mbalimbali wakiwemo viongozi wakuu wa Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar na Waziri wa masuala ya dini wa Saudi Arabia Mhe. Saleh Bin Abdul-Aziz Al ash-Sheikh

Mhe. Rais Magufuli amemuomba Mhe. Saleh Bin Abdul-Aziz Al ash-Sheikh kumfikishia shukrani hizo Mfalme wa Saudi Arabia, Salman bin Abdulaziz Al-Saud kwa msaada huo pamoja na misaada mingine ambayo nchi hiyo imekuwa ikiitoa kwa Tanzania

“Naomba ukamueleze Mfalme kuwa Tanzania inashukuru kwa msaada wa kujenga chuo kikuu na inashukuru kwa ushirikiano mzuri tulionao, sisi Tanzania tutaendeleza ushirikiano huu” amesema Mhe. Rais Magufuli

Katika salamu zake Mhe. Saleh Bin Abdul-Aziz Al ash-Sheikh amempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa uongozi mzuri na hatua kubwa za kimaendeleo ambazo Tanzania imepiga, na amemuhakikishia kuwa Mfalme wa Saudi Arabia anatambua juhudi zinazofanywa na uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano

Nae Mufti wa Tanzania Sheikh Aboubakar Zubeir Ali amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuandaa futari hiyo na kuwakaribisha wageni mbalimbali na ameuelezea ukarimu huo kuwa ni moja ya miongozo mikuu ya dini ya Kiislamu hususani katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhan, pia amemuhakikishia kuwa Waislamu wote wanaungana na juhudi mbalimbali za Serikali pamoja na kuiombea nchi kuwa na amani. 

Viongozi wengine waliohudhuria futari hiyo ni Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Seif Ali Idd, Spika wa Bunge Mhe. Job Yustino Ndugai, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Zubeir Ali Maulid

Wengine ni Mke wa Rais Mhe. Mama Janeth Magufuli, Marais Wastaafu Mhe. Alhaji Ali Hassan Mwinyi na Mhe. Benjamin William Mkapa, Makamu wa Rais Mstaafu Mhe. Dkt. Mohamed Gharib Bilal, Mawaziri Wakuu wastaafu Mhe. Dkt. Salim Ahamed Salim, Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba, Mhe. John Samuel Malecela na Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda.
Rais Magufuli aishukuru Saudi Arabia kwa msa ada wa kujenga chuo kikuu Rais Magufuli aishukuru Saudi Arabia kwa msa ada wa kujenga chuo kikuu   Reviewed by KUSAGANEWS on May 29, 2018 Rating: 5

No comments: