Mahakama ya Hakimu mkazi Kisutu
imeyatupilia mbali maombi ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na wenzake
nane ya kutaka kesi yao iende Mahakama Kuu kwa ajili ya kupata tafsiri ya
kisheria kuhusu uhalali wa kushitakiwa kwa makosa ya jinai wakati wakitekeleza
majukumu yao kikatiba.
Uamuzi huo umetolewa na Hakimu Mkazi
Mkuu, Wilbad Mashauri na kuipanga kesi hiyo ianze kusikilizwa kuanzia Mei
16,2018 saa 8 mchana kwa ajili ya washtakiwa hao kusomewa maelezo ya awali.
Mahakama imetoa uamuzi huo mbele ya
washtakiwa, Freeman Mbowe, Mbunge wa Iringa Mjini Peter Msigwa, Naibu Katibu
Mkuu Zanzibar Salum Mwalimu na Naibu Katibu Mkuu Bara na Mbunge wa Kibamba John
Mnyika.
Wengine ni Mbunge wa Tarime mjini Esterher
Matiko, Katibu Mkuu wa Chama hicho Dkt.Vicenti Mashinji naMbunge wa Tarime
vijijini, John Heche.
Katika kesi hiyo washtakiwa Eshter
Bulaya na Mbunge wa Kawe Halima Mdee hawakuwepo Mahakamani ambapo kwa mujibu wa
wakili wa upande wa utetezi Peter Kibatala ameiambia Mahakama kuwa walipatwa na
tatizo katika gari wakati wakiwa njiani wakitokea Dodoma kuja Dar es Salaam.
Aidha, Kibatala ameiomba Mahakama
kuipanga kesi hiyo kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali Juni 8 ama
15, 2018 ombi ambalo lilipingwa na upande wa mashtaka na kuiomba Mahakama
washtakiwa hao wasomewe maelezo ya awali Mei 16,2018 mwaka huu.
Kutokana na hoja za upande wa
utetezi na mashtaka kuhusu tarehe ya kusomwa kwa maelezo ya awali, Hakimu Mkazi
Mkuu Wilbad Mashauri ameiahirisha kesi hadi mei 16,2018 saa nane mchana ambapo
washtakiwa hao watasomewa maelezo ya awali.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na jumla
ya mashtaka 12 katika kesi ya jinai namba 112 ya mwaka 2018 ikiwamo kula njama,
kufanya mkusanyiko usio halali kinyume cha sheria na kuendelea kufanya
mkusanyiko usio halali ama maandamano yaliyosababisha kifo cha Akwilina.
Maombi ya CHADEMA yatupiliwa mbali
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 15, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment