Ubishani wa kisheria katika kesi inayomkabili Freeman Mbowe
na wenzake wanane uliilazimisha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kufanya kazi
mpaka saa 1:58 usiku kabla ya kuahirishwa hadi Juni 11
Kiini cha ubishani katika kesi hiyo iliyoanza kusikilizwa
saa nane mchana jana ni upande wa utetezi katika kesi hiyo kuwasilisha
pingamizi nane ukiomba mashtaka yanayowakabili washtakiwa yafutwe kwa sababu
yana upungufu kisheria
Wakili wa utetezi Peter Kibatala katika ombi mbadala aliomba
iwapo Mahakama itashindwa kuifuta hati nzima ya mashtaka, basi iyafute ambayo
yana upungufu kisheria
Amedai maelezo kwa shtaka la nne, tano, sita na la saba
yanawachanganya washtakiwa na hawawezi kujitetea kikamilifu
Pia, mashtaka hayo amedai ili kufunguliwa kunahitaji ridhaa
ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ambayo haipo
Wakili Kibatala aliwasilisha pingamizi hizo jana mbele ya
Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri baada ya Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja
Nchimbi kuiambia Mahakama kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya washtakiwa
kusomewa maelezo ya awali na walikuwa tayari kwa kufanya hivyo
Nchimbi baada ya kueleza hayo, Kibatala alisema ni kweli
lakini wamewasilisha pingamizi hizo za kisheria
Kibatala alidai panapokuwa na pingamizi kwa mujibu wa sheria
ni lazima lisikilizwe kwanza. Upande wa mashtaka haukupinga na mahakama
iliridhia
Kibatala alidai kibali kilichotolewa na DPP kuipa ridhaa
Mahakama ya Kisutu kusikiliza kesi hiyo kina upungufu kwa sababu hakisemi
kimetolewa kwa mashtaka yapi na kwamba kimetaja majina ya washtakiwa bila
kufafanua makosa waliyotenda.
“Siyo kazi ya
Mahakama kutafuta mashtaka yanayohusiana na hicho kibali cha DPP, hivyo hoja
yetu hakuna ridhaa ya DPP kwa sababu kibali hicho si sahihi,” alidai Kibatala
Alidai shtaka la nne, tano, sita na saba kufunguliwa kwake
kunahitaji ridhaa ya DPP na kwa kuwa haipo aliomba yafutiliwe mbali.
Kibatala alidai hati
ya mashtaka ina upungufu kwa sababu shtaka la pili na la tatu hayana maelezo ya
kutosheleza ya kuwapa msingi na uwezo washtakiwa kujitetea kikamilifu kijinai.
Alidai katika shtaka la kufanya mkusanyiko bila kibali aliwataja hata watu waliotishiwa
na kwamba wametajwa kwa wingi hivyo haijulikani ni washtakiwa au ni watu
wengine
Kibatala alidai mashtaka yanayowakabili wateja wake
yamejichanganya, hayaonyeshi walisababishaje kifo cha Akwilina Akwilini,
aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) na majeruhi
walijeruhiwa na nani na kwa kutumia nini
“Maelezo ya shtaka yamerundika vitu vingi kiasi kwamba ni
vigumu mtu kujitetea na kwamba unapomshtaki mtu kwa kusababisha kifo ni lazima
utoe maelezo ya kutosha kuonyesha unamaanisha kitu fulani ili mtu aweze
kujitetea,” alidai.
Alidai hati ya
mashtaka ina upungufu kwa kuwa haionyeshi dhumuni la pamoja ambalo washtakiwa
walikutana kulitenda hivyo linawanyang’anya haki ya kujitetea.
Alidai pia kuna
upungufu wa kisheria kwa kuwa mashtaka hayaonyeshi watu waliochochewa kufanya
makosa ni kina nani waliohudhuria mkutano, wakazi wa Kinondoni au wapigakura
bila kujali itikadi zao
Wakili wa Serikali Mkuu, Paul Kadushi alipinga hoja hizo za
utetezi na kuiomba Mahakama itupilie mbali pingamizi hizo
Kuhusu kibali cha DPP kinachoipa Mahakama ridhaa ya
kusikiliza kesi, Kadushi alidai hakuna uamuzi wowote ulioweka msingi kwamba ni
lazima kiwepo au kisiwepo
Akiahirisha kesi hiyo, hakimu Mashauri alisema atatoa uamuzi
kuhusu pingamizi hizo Juni 11, mwaka huu
Mbali na Mbowe ambaye ni mwenyekiti wa Chadema, washtakiwa
wengine ni mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; naibu katibu mkuu wa
chama hicho Zanzibar, Salum Mwalimu; na wa Bara ambaye pia ni mbunge wa
Kibamba, John Mnyika
Wengine ni mbunge wa Tarime Mjini Esther Matiko; katibu mkuu
wa Chadema, Dk Vincent Mashinji; mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche; mbunge
wa Kawe, Halima Mdee na wa Bunda, Ester Bulaya.
Kesi ya kina Mbowe yanguruma mpaka saa mbili usiku Kisutu
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 16, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment