Afisa wa Jeshi la Magereza nchini
Zimbabwe amefunguliwa mashtaka kwa kosa la kumkosea heshima Rais wa nchi hiyo
kwa kuandika ujumbe kwenye mitandao ya kijamii akimpandisha kiongozi wa
upinzani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyosambazwa
na taasisi ya wanasheria ya kutetea haki za binadamu ya Zimbabwe Lawyers for
Human Rights (ZLHR), Mamlaka ya Jeshi la Zimbabwe imemfungulia mashtaka John
Mhlabera na kwamba kazi yake iko hatarini kwa kudaiwa kumuita ‘Rais’, kiongozi
wa upinzani.
Mhlabera anadaiwa kuandika kupitia
mtandao wa Twitter kuwa, “Njoo Chiredzi rais wangu.” Hata hivyo, wakati huo
aliyekuwa anaingia katika eneo hilo la Chiredzi ambaye anadaiwa kuwa alikuwa
anamzungumzia ni kiongozi mkuu wa chama cha upinzani cha Movement for
Democratic Change –Tsvangirai (MDC-T), Nelson Chamisa na sio Rais wa Zimbabwe,
Emmerson Mnangagwa.
“Mamlaka ya Jeshi la Magereza limeeleza kuwa
Mahlabera ameonesha utii kwa Chimisa na kutomtii Rais Mnangagwa. Mamlaka hiyo
imedai kuwa kitendo cha Mahlabera ni kumkosea heshima Mnangagwa na kama afisa
wa jeshi la magereza hakupaswa kufanya kitendo kama hicho,” imeeleza taarifa
hiyo ya ZLHR.
ZLHR imeongeza kuwa imewachagua
wanasheria wake wawili kumsaidia Mahlabera atakapofika mbele ya mahakama
kusikiliza mashtaka dhidi yake. Imeelezwa kuwa tangu mwaka 2010 zaidi ya kesi
200 zimefunguliwa dhidi ya watu waliomkosea heshima rais wa Zimbabwe.
Askari ashtakiwa kwa kumuita mpinzani ‘Rais’ mtandaoni
Reviewed by KUSAGANEWS
on
May 29, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment