Na Lydia Churi, Magreth
Kinabo-Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof.
Ibrahim Hamis Juma amesema Chama cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS) ni taasisi
ya Umma na siyo binafsi hivyo amekitaka kutekeleza majukumu yake ya msingi ya
kisheria kwa kushirikiana na Mahakama na kuacha kujiingiza kwenye masuala ya
uanaharakati na siasa.
Akizungumza na Waandishi wa Habari
leo jijini Dar es salaam Jaji Mkuu amesema TLS ni chama huru cha kitaaluma kwa
kuwa kilianzishwa kwa mujibu wa sheria kufanya kazi kwa manufaa mapana ya Umma.
“Hatuwezi kukubali chama hiki
kikajisemea kuwa wao ni chama binafsi na tukakubali, dhana ya ubinafsi haipo”,
alisisitiza Jaji Mkuu.
Alisema jukumu la TLS ni Kuisaidia
Serikali na Mahakama kuhusu mambo yoyote yanayogusa sheria, utawala wa sheria
na kazi za kisheria na akaongeza kuwa dhana hii ndiyo inayoiunganisha Taasisi
hiyo na Mahakama ya Tanzania.
Aidha, Jaji Mkuu amewataka viongozi
wa TLS kushirikiana na Mahakama pamoja na Mihimili mingine ya dola na
kuacha malumbano kwenye vyombo vya habari kwa kuwa hayawasaidii kuendeleza
chama hiki muhimu kwa wanasheria nchini.
Jaji Mkuu pia amewashauri viongozi
wa chama hicho kumuheshimu Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuwa Sheria na
Kanuni zote ni lazima zipitie kwake.
Alisema Mamlaka ya Baraza la Uongozi
la TLS katika Kutekeleza Majukumu ya Umma ni kusaidia kuboresha elimu ya sheria
na taaluma ya Sheria Tanzania na kuwawezesha wanataaluma wa sheria kupata elimu
ya ziada ya sheria kwa kadri mabadiliko yanayotokea nchini na duniani.
Majukumu mengine ya TLS ni pamoja na
kuwawakilisha, kuwatetea na kuwasaidia wanasheria Tanzania kuhusu mazingira ya
kufanya kazi za kisheria na kuwasaidia wananchi wa Tanzania katika masuala ya
kisheria yanayogusa Sheria.
TLS ni Taasisi iliyoanzishwa kwa
mujibu wa Sheria za nchi kabla ya Uhuru na kukubalika kuendelea kuwepo kama
Taasisi ya Kisheria kwa malengo ya kuanzishwa kwake kuelekezwa kwenye manufaa
ya umma kwa kushirikiana na Mahakama, Bunge, pamoja na Ofisi ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali.
Chama hiki kilianzishwa kwa Sheria
ya Baraza la Kutunga Sheria (Legislative Council) Namba 30 ya 1954 na ni moja
ya Sheria nyingi za iliyokuwa Tanganyika kabla ya Uhuru, ambazo kwa mujibu wa
Kifungu cha 4 cha Katiba ya Tanganyika ziliruhusiwa kuendelea kutumika
Tanganyika ilipopata Uhuru Disemba 9 mwaka 1961 kama Sheria za Tanganyika huru.
TLS Ni Chama Cha Umma Kifanye Kazi Kwa Mujibu Wa Sheria
Reviewed by KUSAGANEWS
on
April 24, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment