Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
imeelezwa kuwa hali ya kigogo wa IPTL, Harbinder Sethi inazidi kudhoofika na
puto alilowekwa tumboni linaweza kupasuka wakati wowote.
Hayo yamedaiwa leo mahakamani hapo
mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi na Wakili wa Sethi, Hajra Mungula
ambapo amedai puto hilo linaweza kupasuka na kuhatarisha maisha yake.
Wakili Mungula aliutaka upande wa
mashtaka kueleza upelelezi wa kesi hiyo umefikia katika hatua gani kwa sasa
kwani Aprili 11, ilitolewa amri ya mahakama Sethi apelekwe katika
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya matibabu.
“Nashukuru Aprili 18,2018 mshtakiwa
alipelekwa Muhimbili, akafanyiwa kipimo cha CT-Scan ya tumboni na alipaswa
kupelekwa hospitalini hapo siku inayofuata kwa ajili ya kupatiwa majibu lakini
hadi leo hajapelekwa,” amedai.
Baada ya kusikilizwa hoja hizo,
Hakimu Shaidi alisema amefurahishwa Sethi kupelekwa hospitali ili apatiwe
matibabu na kuamuru apelekwe tena mapema kwa sababu ya afya yake.
Aliamuru upande wa mashtaka kufanya
kadiri wawezavyo kukamilisha upelelezi. Kesi imeahirishwa hadi Mei 10,2018 kwa
ajili ya kutajwa ili kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika au la.
Sethi na mfanyabiashara James
Rugemarila, wanakabiliwa na mashtaka 12 ya uhujumu uchumi, utakatisha fedha na
kuisababisha Serikali hasara ya Dola za Marekani 22, 198,544.60 na Sh
bilioni 309.
Puto Alilowekewa Tumboni Kigogo IPTL Hatarini Kupasuka
Reviewed by KUSAGANEWS
on
April 25, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment