Kiwango cha malaria kimeshuka


Maambukizi ya ugonjwa wa Malaria nchini yameshuka kwa nusu zaidi  kutoka asilimia 14. 4 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 7. 3 mwaka 2017.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakati wa maadhimisho ya siku ya Malaria Duniani ambayo yamefanyika leo Wilayani Kasulu katika Mkoa wa Kigoma.

"Katika kuhakikisha tunatokomeza kabisa ugonjwa huo Wizara ya Afya kupitia Bohari Kuu ya Dawa (MSD) tumepokea na kusambaza vitendanishi vya malaria (mRTD) , vipimo 21, 428, 725, dawa za mseto dozi 12, 916, 050 kwa ajili ya maralia isiyo kali, sindano za kutibu malaria kali vichupa 1, 668, 464 na vidonge vya SP dozi 6, 899, 700 kwa ajili ya tiba kinga dhidi ya athari za malaria wakati wa ujauzito" amesema Waziri Ummy.

Aidha Waziri Ummy amesema kuwa ili watanzania tuendelee kutokomeza kabisa ugonjwa wa malaria tunatakiwa kushiriki kikamilifu katika kutumia afua zote za kupambana na ugonjwa huo ikiwemo kunyunyizia viuadudu vya kuua viluilui vinavyoweza kuleta malaria.
Vilevile Waziri Ummy amesisitiza kuwa kila Halmashauri kuunda kamati zitakazohamasisha usafi wa mazingira  ili kuondoa mazalia ya mbu katika kutokomeza malaria.

Sambamba na hilo Waziri Ummy amezindua takwimu za  ugonjwa wa Malaria nchini ambao umefanywa na Taasisi ya Takwimu nchini (NBS) ambayo ndio Takwimu itayotumika na Serikali ya Tanzania.

Kwa upande wake  Waziri Wa Elimu, Sayansi na Mafunzo ya Ufundi Prof. Joyce Ndalichako amesema kuwa atahakikisha wanafunzi wanapambana na ugonjwa wa malaria kwa kuweka somo la afya kwa shule zote za msingi na sekondari nchini.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu Emamanuel Maganga ametoa wito kwa wakazi wa kigoma kutumia vyandarua kwa matumizi sahihi na siyo kinyume na hapo ikiwemo kufungia kuku na kuvulia samaki.

Maadhmisho ya Malaria nchini mwaka huu yamefanyika wilaya ya Kasulu Mkoani kigoma ikiwa imebeba kauli mbiu isemayo "NIPO TAYARI KUTOKOMEZA MALARIA WEWE JE?

Kiwango cha malaria kimeshuka Kiwango cha malaria kimeshuka Reviewed by KUSAGANEWS on April 25, 2018 Rating: 5

No comments: