Imani za kishirikina zaiponza Simba


Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeipiga faini ya jumla ya milioni 1.5 vinara wa michuano ya ligi kuu Simba SC kutokana na makosa mbalimbali ikiwemo la kuonyesha vitendo vinavyoashiria imani za ushirikina kati mchezo wake dhidi ya Njombe Mji uliofanyika Aprili 3, 2018 

Hayo yamebainishwa na taarifa zilizotolewa na MAtendaji mkuu wa Bodi Ligi Boniface Wambura na kusema Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi (Kamati ya Saa 72) ya Bodi ya Ligi katika kikao chake kilichopita kiliweza kupitia taarifa na matukio mbalimbali na kukuta baadhi ya vitu vikiwa vimetendeka ndivyo sivyo nakuamua kutoa maamuzi mbalimbali.

"Simba imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na kuonyesha vitendo vinavyoashiria ushirikina katika mechi iliyofanyika Aprili 3, 2018 kwenye Uwanja wa Sabasaba mjini Njombe, ikiwemo pia mshabiki mmoja wa timu hiyo kuingia uwanjani na kuchukua taulo la kipa wa Njombe Mji lililokuwa golini. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 42(1) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Klabu", amesema Wambura.

Aidha, Wambura amesema katika mechi namba 165 iliyowakutanisha Mtibwa Sugar na Simba nayo wametozwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na mashabiki wake kuingia uwanjani baada ya filimbi ya mwisho ya mechi hiyo kupulizwa na muamuzi iliyofanyika Aprili 9, 2018 kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Timu ya Simba pia imepigwa faini nyingine ya ya sh. 500,000 (laki tano) kwenye mchezo namba 200 uliokuwa unawakutanisha na Tanzania Prisons kutokana na kuwakilishwa na maofisa watatu badala ya wanne kwenye kikao cha maandalizi ya mechi 'pre match meeting' katika mechi hiyo iliyofanyika Aprili 16, 2018 kwenye uwanja wa Taifa, Jijini Dar es Salaam.

Imani za kishirikina zaiponza Simba Imani za kishirikina zaiponza Simba Reviewed by KUSAGANEWS on April 26, 2018 Rating: 5

No comments: