Wakati polisi
wakitoa tahadhari kwa wananchi kuhusu maandamano yaliyoratibiwa kwenye mitandao
ya kijamii na kupangwa kufanyika leo, Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Dk
Wilbrod Slaa amesema ofisi yake ilipokea barua kutoka polisi wa nchi hiyo
kuhusu taarifa za Watanzania waliotaka kuandamana jana.
Hata
hivyo, hapa nchini polisi imeonya ikisema maandamano hayo ni batili na
atakayeshiriki atashughulikiwa.
Akizungumza
na gazeti hili kutoka nchini Sweden, Dk Slaa alisema jana kuwa, polisi walisema
wameshawapa kibali waandamanaji na watawapa ulinzi unaostahili.
“Ilipofika
saa tatu asubuhi, walifika watu kumi, polisi hawakuwa na kazi kubwa
waliwapangia wapi wasimame, walikuja na mabango yao. Lakini hakukuwa na muziki
kwa sababu huku hawatakiwi kupiga muziki,” alisema.
Alisema
baada ya kuwaona waandamanaji hao wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali,
walikubaliana na polisi kuwa waingie ndani ili kujua nini wanachohitaji.
“Walikataa
kuingia ndani na wakasema hawana sababu ya kujadiliana. Tukawaambia tunawaomba
watupe viongozi wawili ili wawe wawakilishi na viongozi hao waseme nini
wanachotaka. Lakini pia walikataa,” alisema.
Dk
Slaa alisema Sweden ni moja ya nchi zenye vyama vya Watanzania vilivyosajiliwa
kuanzia ngazi ya mkoa na kuendelea na viongozi wa vyama hivyo walipiga simu
ubalozini wakimsifu Rais Magufuli.
“Nimepokea
simu kutoka sehemu mbalimbali, kwamba wanamuunga mkono Rais John Magufuli.
Wanataka Rais asilegeze kamba katika vita dhidi ya rushwa na matumizi mabaya ya
mali za umma kwa sababu vita hivyo vinatengeneza maadui ndiyo maana mambo kama
haya yanatokea,” alisema.
Kuhusu
ujumbe aliosema ni wa upotoshaji ulioandikwa kwenye mabango ya waandamanaji
hao, Balozi Slaa alisema unamhukumu Rais kwa mambo ambayo mahakama haijathibitisha.
Akizungumza na waendesha
bodaboda jana, kaimu kamanda wa polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Sweetbert Njolike alisema jeshi hilo limejipanga kuhakikisha kila mtu anafanya
shughuli zake kama kawaida bila uvunjifu wowote wa amani.
“Niwahakikishie
Jeshi la Polisi tumejipanga na mkoa wetu utaendelea kubaki salama hakuna
maandamano yatakayofanyika, hivyo kila mtu aendelee na shughuli zake kama
kawaida,” alisema.

Wakati hayo
yakijiri Dar es Salaam, polisi mkoani Mwanza walifanya onyesho la utayari wa
kiutendaji na vifaa vyao kwa kuzunguka mitaa kadhaa jijini humo.

Msafara
wa magari zaidi ya 15 yaliyokuwa yamewasha taa na kupiga ving’ora ulihusisha
askari wenye sare za kikosi cha kutuliza ghasia (FFU), waliobeba silaha na
kujihami kwa zana na vifaa vya kudhibiti na kukabiliana na ghasia. Miongoni mwa
magari yaliyozungushwa mitaani ni ya doria ya kila siku, gari la maji ya
kuwasha na malori, yote yakiwa na askari.

Kamanda
wa polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema wamejiandaa kikamilifu
kukabiliana na kuwadhibiti wote watakaothubutu kujitokeza mitaani leo kushiriki
maandamano yanayohamasishwa kupitia mitandao ya kijamii.
“Kutakuwa
na doria ya askari wenye sare na wasio na sare mitaani na maeneo yote ya Mkoa
wa Mwanza, watakaothubutu kuandamana watasimulia wengine kitakachowapata,”
alisema.
Mkuu wa mkoa huo, John
Mongella aliunga mkono kauli hiyo akisema maandamano hayo ni haramu kisheria
kwa sababu hadi leo hakuna taarifa iliyotolewa polisi kwa mujibu wa
sheria.
Kutoka Dodoma polisi walipita
mitaani baadhi wakiwa kwenye magari na wengine wakikimbia.
Kamanda
wa polisi mkoani humo, Gilles Muroto alisema watakaothubutu kuandamana
watakabiliwa na jeshi hilo ipasavyo.
Mkoani
Mtwara, kamanda wa polisi wa mkoa huo, Lucas Mkondya alisema watu wachache
wanaohamasisha maandamano wasithubutu kuandamana kwa kuwa watapambana na nguvu
ya dola na madhara yatakayotokea jeshi hilo lisilaumiwe.
Alisema
katika kufuatilia wanaochochea, kuyahamasisha na kumkashifu Rais, wanafunzi
tisa wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine tawi la Mtwara wanashikiliwa.
“Wawili
kati yao upelelezi tumekamilisha na kuwafikisha mahakamani, waliobakia
tunaendelea kukamilisha upelelezi,” alisema.
Kwa
upande wa Morogoro, mkuu wa mkoa huo, Dk Stephen Kebwe alivitaka vyombo vya
ulinzi na usalama kushirikiana kudhibiti maandamano yasiyo halali yaliyopangwa
kufanyika leo.
“Kama kuna watu
wanataka kuandamana basi wajifungie chumbani waandamane lakini wakijaribu
kuingia barabarani polisi hakikisheni mnawashughulikia,” aliagiza Dk Kebwe.
Kamanda
wa polisi mkoani humo, Ulrich Matei alisema kwamba wapo askari na vifaa vya
kutosha kukabiliana na maandamano hayo.
Wakati huohuo, baadhi ya
Watanzania wanaoishi nchini Marekani waliandamana hadi katika ofisi za ubalozi
wa Tanzania mjini Washington kuwasilisha madai yao.
Baadhi
ya picha zilizotumwa kwenye mitandao ya kijamii ziliwaonyesha waandamanaji hao
wakiwa na mabango wakiwa nje ya ubalozi huo huku wengine wakisikika
wakizungumza mambo mbalimbali.
Baadaye
watu hao waliokuwa wakizungumza Kiswahili walijipanga kando ya barabara
wakiimba na kuendelea kuonyesha mabango yao.
Imeandikwa
na Fortune Francis, George Njogopa (Dar), Saada Amiri (Mwanza), Florah Temba
(Moshi), Hamida Shariff (Morogoro) na Haika Kimaro (Mtwara).
Dk Slaa azungumzia maandamano nchini Sweden, polisi waonya
Reviewed by KUSAGANEWS
on
April 26, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment