Jeshi la Uhamiaji Mkoa wa Kilimanjaro,
limebaini mbinu mpya wanayotumia mawakala kusafirisha wahamiaji haramu ambapo
kwa sasa wanawabadili mwonekano kwa kuwanyoa vipara na kuwavisha mavazi
yanayotumiwa na kabila la kimasai ili kuvikwepa vyombo vya sheria.
Katika kipindi cha Januari 2017 hadi Machi
22,2018, jeshi hilo limewakamata wahamiaji haramu 208, katika maeneo mbalimbali
mkoani Kilimanjaro, kwa tuhuma za kuingia nchini, kinyume cha sheria
Akizungumza ofisini kwake leo Machi 23 Mkuu
wa Uhamiaji Kilimanjaro, Naibu Kamishna wa Uhamiaji Albert Rwelamira, amesema
Machi 22 mwaka huu, waliwakamata watu wawili katika mpaka wa Holili,
akiwemo raia mmoja wa Ethiopia, ambaye alikuwa amevalia mavazi ya kimasai huku
akiwa amenyoa upara kwa lengo la kukwepa vyombo vya ulinzi maeneo ya mpakani
Aliwataja watu waliokamatwa kuwa ni Saimon
Ngarieni Kalanga (28)Masai, mkazi wa Simanjiro mkoani Manyara, ambaye alikuwa
akimsafirisha Kibamo Gashe Abate (26) Raia wa Ethiopia, kwenda nchini Afrika
Kusini
“Katika kupambana na wahamiaji haramu, tuna
mitandao tunayoifuatilia, na tumebaini njia wanazozitumia ili kutukwepa kwani
awali walikuwa wakipita vichochoroni, lakini kwa sasa wanawabadilisha
muonekano, wanawanyoa nywele zote na kubaki upara na kuwavisha mavazi ya kimasai (rubega) ili kutukwepa,” amesema
Rwelamira
Amesema Mtanzania ambaye alikuwa
akimsafirisha raia huyo wa Ethiopia, mbali na kumbadilisha muonekano, pia
alimbadilisha jina na kumpa majina ya Samuel ili kumficha katika basi
walilokuwa wakisafiria asifahamike kiurahisi
Kwa mujibu wa Kamishna Rwelamira raia huyo
wa Ethiopia, alikuwa na hati ya kusafiria namba Ep 50554339, ambayo inaonyesha
kutolewa Februari 22 mwaka huu nchini Ethiopia na alitoka nchini humo Machi
Mosi mwaka huu akipitia nchini Kenya, ambapo iligongwa muhuri lakini alipofika
Tanzania hakuitumia kutokana na utaratibu wa viza uliopo ambao wanadai ni mgumu
“Tunaendelea na jitihada za kupambana na
mtandao wa kusafirisha wahamiaji haramu ambao unaonekana kuwezeshwa na baadhi
ya Watanzania kwani mawakala wa usafirishaji wapo kuanzia Ethiopia kwenyewe
Kenya, Tanzania, Zimbabwe hadi Afrika Kusini, na hapa unaweza kuona ni kiasi
gani cha fedha wanachotumia katika kazi hii.”
Pia alisema katika kupambana na hali hiyo
tayari wamezungumza na wawakilishi wa kampuni za magari, kuwataka kuwa makini
hasa wakati wa ukataji wa tiketi na kuhakikisha wale wanaofika kuwakatia watu ambao hawapo, wanafika na vitambulisho vyao
vyenye picha ili kujiridhisha
Alisema kwa mujibu wa sheria likikamatwa
gari lililobeba mhamiaji haramu linatakiwa kutaifishwa hivyo ni vyema wakawa
makini na kuhakikisha wanatoa taarifa pindi anapoingia mtu kwenye gari na kumtilia shaka
“Lazima wajiulize, mtu anayekuja kukata
tiketi ya watu wawili au watatu na watu hao hawapo, hivyo wahakikishe wanakuja
na vitambulisho vyao vyenye picha ili kujiridhisha kama majina yanafanana,
watusaidie katika hili, wasiangalie maslahi ya kibiashara, waangalie maslahi ya
taifa na usalama wa nchi”
Wahamiaji haramu wabadili Mfumo waja kimasai
Reviewed by KUSAGANEWS
on
March 23, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment