Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema),
Godbless Lema amesema uhusiano usioridhisha kati ya wabunge na viongozi wa
Serikali unakwamisha shughuli za maendeleo.
Mbunge huyo ameshauri itafutwe
suluhu ili kurejesha mahusiano mazuri baina ya makundi hayo.
Akizungumza leo katika kikao
cha kamati ya ushauri ya mkoa wa Arusha, Lema amesema kama hakuna mahusiano
mazuri kwa viongozi si rahisi kuwapatia wananchi maendeleo
"Hili ni suala la utawala
bora, leo hii kuna watendaji wa Serikali wanaogopa hata kupiga picha na
wabunge, hasa wa upinzani. Jambo hili linapaswa kuondolewa kwani lina athari
katika jamii,” amesema Lema
Amesema wabunge wana nafasi ya
kuchochea maendeleo ya wananchi na kuondoa kero zao, kwamba kuna wakati
kiongozi wa serikali kutokana na sababu za kiitifaki hawezi kupeleka
hoja moja kwa moja kwa viongozi wa juu lakini mbunge anaweza
"Tufanye kazi pamoja, leo hii
tunapitisha bajeti ya mkoa lakini kama hatuna mahusiano mazuri baina
yetu, sisi kama viongozi sidhani kama tutafanikiwa,” amesema.
Akijibu hoja hiyo ya Lema Kaimu
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Idd Kimanta amesema anaamini viongozi wa
Serikali wanajua wajibu wao wa kufanya kazi na wadau mbalimbali
"Utawala bora ni pamoja na
kufanyakazi pamoja na nina imani hili linafanyika lakini kama kuna watu
wanatengwa hilo ni jambo la watu binafsi,” amesema.
Hata hivyo, Kimanta ametaka
viongozi kufanya kazi ya kutatua kero za wananchi na kuachana na mambo ya
siasa kwani chaguzi tayari zimepita sasa ni wakati wa kufanyakazi.
|
UHUSIANO USIORIDHISHA KATI YA VIONGOZI WA SERIKALI UMEKWAMISHA MAENDELEO
Reviewed by KUSAGANEWS
on
March 10, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment