|
|||
Umoja wa madereva wanaosafirisha magari nje ya nchi
(ITDA) wameiomba Serikali kufikiria kutunga sheria ndogo ili kulinda ajira za
wazawa kufuatia kazi nyingi kuchukuliwa na wageni.
Kilio hicho kimetolewa leo Machi 10, 2018 wakati wa
mkutano mkuu wa mwaka wa umoja huo ambao ulilenga kujadili masuala mbalimbali
ikiwemo uhakika wa ajira zao.
Madereva hao wamelalamika kuwa raia wa kigeni wamekuwa
wakichukua ajira hizo za kupeleka magari katika nchi zao huku Watanzania
wakibaki wanyonge.
Mmoja wa madereva hao, Peter Mhina amesema hivi sasa
imekuwa kawaida magari yanapotoka bandarini kuendeshwa na dereva wa
nchi husika linakokwenda
Amesema hali hiyo imekuwa kikwazo kikubwa cha ajira
kwa wazawa ambao wamekuwa wakitegemea kupata kazi za kusafirisha magari hayo
na hivyo kujiongezea kipato
"Hali imekuwa mbaya bandari yetu lakini tunaishia
kuangalia maji, wenzetu kazi wanapeana wenyewe kwa wenyewe, ukifuatilia kwa
undani madereva wengi sasa hawana kazi," amesema Mhina.
Mwenyekiti wa ITDA, Jimmy Mwalugelo amekiri kuwepo kwa
changamoto hiyo na kueleza kuwa jitihada zinaendelea kufanyika kupata
ufumbuzi.
Amesema hali hiyo ni matokeo ya makubaliano ya
ushirikiano kati ya Tanzania na nchi nyingine za Afrika Mashariki hivyo ni
muhimu kuheshimu makubaliano hayo
"Hatuwezi kukiuka makubaliano ya ‘protocol’ namba
13, hiyo ndiyo inawapa nguvu wenzetu kuchangamkia fursa hiyo ya
ajira," amesema
Amesema ili kupata ufumbuzi ni muhimu Serikali
ikaanzisha sheria ndogo itakayoelekeza magari yote yanayotoka bandarini
yaendeshwe na dereva aliyepitia mafunzo maalum yatakayotolewa katika Chuo cha
Muhonda
"Tunafanya utaratibu wa kuanzisha chuo, ambacho
kitakuwa kinatoa mafunzo mafupi na yenye tija kwa madereva
wanaokwenda nje ya
nchi, hawa tutawapatia vyeti,"amesema
“Ndiyo sababu tunashauri kwa kusaidia kulinda ajira za
wazawa iwekwe sheria itakayomtaka dereva anayetoa gari bandarini awe na cheti
hiki pamoja na leseni."
Amesema mataifa ya jirani yamechangamkia fursa ya
ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa kuwaweka watu wao kufanya kazi mipakani
na bandarini.
Pamoja na hilo amewasisitizia madereva umuhimu wa kuwa
na bima za afya ili kuwa na uhakika wa matibabu yao na familia zao
"Hizi kazi hazieleweki unaweza ukasafiri ukapata
matatizo njiani au familia yako ikapata matatizo ukiwa na bima ni nafuu
unatibiwa hata kama huna fedha kwa wakati huo," amesema.
|
|||
|
|||
MADEREVA WANAOSAFIRI NJE YA NCHI WAIOMBA SERIKALI ITUNGE SHERIA YA WAZAWA
Reviewed by KUSAGANEWS
on
March 10, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment