Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk
Hamisi Kigwangalla amemsimamisha kazi mkuu wa kanda Pori la Akiba Rukwa
lililopo wilayani Mlele mkoani Katavi kupisha uchunguzi wa tuhuma
zinazomkabili.
Taarifa ya Kaimu Katibu Mkuu, Dk Aloyce
Nzuki iliyotolewa jana Machi 10,2018 inasema waziri amemsimamisha kazi Emmanuel
Barabara ambaye pia ni mhifadhi wanyamapori mkuu.
Dk Kigwangalla amefikia uamuzi huo
kutokana na taarifa za raia wema kuwa Barabara amekuwa akishirikiana na
majangili kuhujumu rasilimali za misitu nchini.
Waziri Kigwangalla katika taarifa
hiyo ameagiza iundwe kamati ya uchunguzi kubaini ukweli wa tuhuma hizo.
Amesema iwapo mtuhumiwa atatiwa
hatia, hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za
utumishi wa umma ili iwe fundisho kwa wengine.
Tunatoa onyo kali kwa watumishi wa
wizara wanaojihusisha na vitendo vya uhujumu wa rasilimali za misitu,
wanyamapori na mali kale. Tunawataka waache mara moja kwa kuwa hatutosita
kuchukua hatua kali za kinidhamu kwa yeyote atakayebainika kujihusisha na
vitendo hivyo, ikiwemo kufukuzwa kazi,” amesema.
Amewataka watumishi wa wizara
kuzingatia sheria, kanuni, utaratibu na miongozo iliyowekwa katika utekelezaji
wa majukumu yao ya kila siku ya uhifadhi wa rasilimali za nchi kwa faida ya
kizazi cha sasa na kijacho.
KIGWANGALA AMSIMAMISHA KAZI MKUU WA KANDA
Reviewed by KUSAGANEWS
on
March 11, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment