Mgogoro baina ya wakazi wa Kijiji cha
Mapangoni wilayani hapa na Jeshi la Magereza umeingia katika sura nyingine
baada ya Serikali kuingilia kati na kukanusha uvumi ulioenea kwamba askari 11
waliopo mahabusu wametoroka.
Serikali imesema askari hao wanaotuhumiwa
kwa mauaji ya mkazi wa kijiji hicho, Aloyce Makala (41) wapo mahabusu
wakisubiri kesi yao kusikilizwa na kutolewa hukumu na kuwataka wananchi kuacha
kusikiliza maneno ya mitaani badala yake wasubiri mahakama ifanye kazi yake
Kaimu mkuu wa wilaya ya Korogwe, Godwin Gondwe alifanya
ziara kijijini hapo kwa lengo la kutatua mgogoro huo ambao uliibuka baada ya
kutokea mauaji hayo Januari 22 mwaka huu
Alisema kuwa askari wote 11 wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya mwananchi huyo wapo kwenye mikono ya sheria na tayari wameshafikishwa mahakamani
Aliwataka wakazi wa kijiji hicho wasiichukie
taasisi ya magereza kuwepo kwenye eneo hilo kwani ipo kwa ajili ya
manufaa yao ila wale ambao wamehusika kuharibu amani kwa wananchi
wameshafikishwa kwenye vyombo vya dola
"Serikali haiangalii wadhifa wa
mtu katika uwajibikaji, yeyote atakaekosea sheria itafuata mkondo wake na
ikibainika amefanya makosa hatua za kisheria dhidi ya mhusika lazima
zichukuliwe," alisema Gondwe.
Aliwataka wananchi wa kijiji cha Mapangoni
kuhakikisha kuwa na uhusiano mzuri na Jeshi la Magereza kwani si
wote waliohusika katika hilo suala lililotokea
Diwani wa kata ya Kelenge, Shebila Saidi
alisema kutokana na tukio hilo, ni vyema kwa sasa taasisi hiyo ya magereza
kuondoa kambi yao iliyopo kwenye kijiji cha Mapangoni ili kuweza kuwepo amani na ushirikiano mzuri kwani bado wapo wananchi
wenye kinyongo
Alisema tukio lililotokea limeleta taswira
mbaya miongoni mwa wananchi hivyo kwa muda magereza wahamishe taasisi yao irudi
makao makuu ya Korogwe hadi pale vuguvugu hilo litakapopatiwa
Mmoja wa wananchi wa kijiji cha Mapangoni,
Mashaka Mussa alisema mara kwa mara kumekuwepo na mahusiano yasiyoridhisha
baina ya askari hao na wananchi ambapo hata yeye alishagombana na askari
magereza wawili kwa kukatiwa migomba yake shambani na alipokwenda baraza la
ardhi alishinda kesi
Hata hivyo kaimu mkuu wa jeshi la polisi wilaya ya Korogwe Saidi Mwagara aliwataka wananchi wa eneo hilo kuhakikisha wanalinda amani yao kwa kukwepa vitu ambavyo vinasababisha ukosefu wa amani kwani ni rahisi kuondoa amani ila si kuirudisha
Askari wa Jeshi la Magereza waliofikishwa mahakamani hapo kwa shitaka hilo ni Jonas Makere, Shadrack Lugendo, Razalo Stephen, Musa Zuberi, Ramadhan Yusuf, Robert Alfred, Fredrick Osmas, Alfonce Revocatus, Mbesha Naftari, Hamis Msola na Michael Elia.
GODWIN GONDWE ATATUA MGOGORO
Reviewed by KUSAGANEWS
on
March 23, 2018
Rating:
No comments:
Post a Comment