Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William
Lukuvi amepokewa kwa mabango na wakazi wa Kijiji cha Rwakalemela kilichopo Kata
ya Kasulo, Wilaya ya Ngara mkoani Kagera wakimuomba kutatua migogoro ya ardhi.
Wananchi hao walitoa ombi hilo kwa Lukuvi leo Februari 22,
2018 baada ya waziri huyo kufika wilayani humo akitokea Karagwe akiwa
katika ziara ya kiutendaji mkoani Kagera
Waziri huyo baada ya kufanya kikao cha ndani na viongozi wa
wilaya alisikiliza kero za wananchi wa wilaya hiyo kuhusu migogoro ya ardhi
katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Rwakalemela Wananchi
hao waliokuwa wamebeba mabango yenye ujumbe mbalimbali wa kutaka migogoro ya
ardhi kutatuliwa, wengi walimuomba waziri huyo kuwafutia hatimiliki wenye
mashamba makubwa waliyoyapata bila kufuata utaratibu wa Sheria ya Ardhi namba 5
ya mwaka 1999
Mmoja wa wananchi hao, Amiri Rashidi amesema baadhi ya
wananchi waliowahi kuwa viongozi wa chama na serikalini na pia wenye uwezo wa
kifedha walijimilikisha mashamba makubwa katika kata za Kasulo, Kabanga
na Rulenge na kusababisha wananchi wengine kukosa mashamba.
Kitendo cha Rashidi kuzungumza huku akitokwa na machozi
kilimwamsha kwenye kiti Ofisa Ardhi wa Wilaya ya Ngara, Betty Munuo kutoa
maelezo kuhusu mzee huyo kwamba, eneo lake alilimiliki mwaka 1969, lakini
tangu mwaka 1985 lilichukuliwa na kuwa kituo cha kuegesha magari
“Huyu anastahili kulipwa tangu mwaka 1985, hivyo anastahili
kulipwa na ofisi ya mkurugenzi ambayo haijatekeleza maagizo ya mahakama.
Baadhi ya wananchi waliwataja vigogo waliojimilikisha
mashamba ambao kutokana na kutowapata majina yao yamehifadhiwa.
Awali, Mbunge wa Ngara, Alex Gashaza amesema migogoro ya
ardhi wilayani humo ni mingi na wenye uwezo ndio wanaowanyanyasa wananchi
masikini.
Katika ufafanuzi wake, Lukuvi amesema Serikali inafanya
mpango wa kurekebisha utaratibu wa kutatua migogoro ya ardhi kwa kubadilisha
mfumo wa mabaraza ya ardhi kwa kila kata
“Migogoro ya ardhi ambayo imefikishwa mahakamani waziri hana
mamlaka ya kuingilia, lakini naagiza mwanasheria wa halmashauri hakikisha
wajumbe wa mabaraza ya ardhi ambao si waaminifu wanaondolewa kwenye mabaraza
hayo ili haki iweze kutendeka,” amesema Lukuvi.
Lukuvi apokewa kwa mabango Ngara inayotokana na migogoro ya Ardhi
Reviewed by KUSAGANEWS
on
February 22, 2018
Rating:

No comments:
Post a Comment