Maombi ya dhamana ya
wabunge wawili wa Chadema na washtakiwa wengine 37 yamekwama kusikilizwa
ikielezwa hakimu anaumwa.
Katika Mahakama ya
Hakimu Mkazi Morogoro, imeelezwa hakimu Ivan Msack anayesikiliza kesi hiyo ni
mgonjwa hivyo imeahirishwa na washtakiwa wamepelekwa rumande hadi Desemba
8,2017.
Akiahirisha kesi hiyo
leo Jumatano Desemba 6,2017, hakimu Erick Rwehumbiza amesema Msack amepata
maradhi ghafla na yuko hospitalini kwa matibabu.
Baada ya kuelezwa
mahakamani kuwa hakimu ni mgonjwa, upande wa utetezi ulimuomba Rwehumbiza kesi
hiyo ihamishiwe kwa hakimu mwingine.
Wakili wa utetezi,
Peter Kibatala amesema kuahirishwa kesi hiyo na kutotolewa dhamana kwa
washtakiwa kunalenga kuchelewesha upatikanaji wa haki.
Kibatala pia ameiomba
Mahakama iruhusu wananchi kuingia ndani ya ukumbi kufuatilia uendeshaji wa kesi
hiyo.
Wakili wa Serikali,
Sunday Hyera akizungumzia hoja ya wananchi kuruhusiwa kuingia ndani ya ukumbi
wa Mahakama amesema haina msingi katika kesi hiyo na hakuna uwezekano wa
kuiwasilisha mahakamani.
Hakimu Rwehumbiza
akijibu hoja hizo, amesema alipewa jalada la kesi kwa ajili ya kuiahirisha.
Kuhusu dhamana amesema
ombi hilo litashughulikiwa na hakimu anayehusika na iwapo hatakuwepo Desemba
8,2017 wataangalia namna ya kuihamishia kwa hakimu mwingine.
Hakimu Rwehumbiza
amesema suala la wananchi kuingia mahakamani haliathiri uendeshaji wa kesi kwa
kuwa wanaweza kuwepo wawakilishi wao.
Wabunge Susan Kiwanga
wa Mlimba na Peter Lijualikali wa Kilombero na washtakiwa wengine walifikishwa
mahakamani Novemba 30,2017 wakidaiwa Novemba 26,2017 katika Kata ya Sofi wilayani
Malinyi walifanya uharibifu wa mali.
Wanadaiwa bila
uhalali, huku wakijua wanatenda kosa walikula njama na kuchoma moto ofisi ya
kata na kufanya uharibifu wa mali.
Hakimu alisema angetoa
uamuzi wa dhamana jana Desemba 5,2017 lakini hilo halikufanyika kutokana na
kuibuka hoja za kisheria kuhusu hati ya kiapo ya kupinga dhamana
iliyowasilishwa mahakamani hapo.
Kutokana na mvutano wa
kisheria, hakimu Msack aliahirisha kesi hiyo hadi leo Jumatano Desemba 6,2017
ili kutoa fursa kwa pande zote mbili kujibu hoja kuhusu hati hiyo.
Wabunge wa CHADEMA warudishwa Tena rumande, hakimu anaumwa
Reviewed by KUSAGANEWS
on
December 06, 2017
Rating:

No comments:
Post a Comment