Jeshi la Ulinzi wa
Wananchi wa Tanzania limesema kikundi chake cha ulinzi na usalama kilichopo DRC
kwaajili ya kutekeleza jukumu la ulinzi na amani kilivamiwa na Waasi
waliojilikana kuwa ni ADF na kusababisha mauaji kwa wanajeshi 14.
Amesema kwamba tukio hilo lilitokea
katika eneo la kambi iliyopo daraja kwenye mto Simulike barabara ya kutokea
Oicha kwenda Kamango mpakani mwa nchi ya Uganda Kaskazini Mashariki ya wilaya
ya Beni Jimbo la Kivu Kaskazini.
Akithibitisha mauaji hayo muwakilishi
wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama
Tanzania (CDF) Luteni Jenerali James Mwakibolwa amesema
shambulio hilo lakuvamiwa lilizusha mapigano baina ya kikundi hicho na kile cha
waasi na yalidumu kwa takribani masaa kumi na tatu (13) na kusababisha vifo vya
askari wa Tanzania 14 na wengine 44 kujeruhiwa na askari wawili bado
hawajulikani walipo ambapo jitihada zaidi za kuwatafuta zinaendelea.
Amesema shambulizi la tarehe 7
kuamkia tarehe 8 Desemba lilikua baya zaidi kuwahi kuitokea tangu vikosi
hivyo vianze kushiriki ulinzi wa amani nchini DRC mwaka 2011 kwakua
limeleta madhara makubwa, hata hivyo kikundi hicho ambacho bado kipo huko
kinauwezo mkubwa wa kutekeleza majukumu husika kwa uhodari wa hali ya juu
,ushupavu, weledi mkubwa na umahiri stahiki.
Kwa niaba ya mkuu wa
majeshi Luteni Jenerali Mwakibolwa amewathibitishia watanzania kuwa tukio
hilo halitawavunja moyo na kamwe Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania
halitatetereka kupeperusha bendera yake ndani na nje ya nchi kwani tukio hilo
limewaongezea nguvu, ari ,ushupavu na uhodari zaidi katika kutekeleza majukumu
yake.
Aidha amesema nchi pia iko salama na
itaendelea kuwa salama na yeyote ambaye anataka kuwajaribu atashughulikiwa
ipasavyo kwani historia ya jeshi inadhihirisha uwezo thabiti.
Kuhusu taratibu za kusafirisha miili
ya marehemu kuirejesha nchini zinafanyika chini ya utaratibu wa Serikali na
umoja wa mataifa na JWTZ na serikali wanaendelea kuchukua hatua stahiki
kufuatia tukio hilo ikiwemo kufanya uchunguzi katika eneo husika sambamba na kuangalia
taratibu za kuwajulisha familia za wafiwa zimekamilika na ndio maana hawakuweza
kutoa taarifa hizo bila kuwaweka sawa familia za mashujaa hao.
Kwa umoja wa watanzania amewataka
kuwaombea dua roho za mashujaa hao zipumzike mahali pema peponi kwa amani na
majeruhi wote wapone haraka iwezekanavyo ili warejee kutekeleza majukumu yao ya
kila siku kwa ulinzi wa taifa na dunia nzima.
JWTZ wazungumzia vifo vya Wanajeshi 14
Reviewed by KUSAGANEWS
on
December 10, 2017
Rating:

No comments:
Post a Comment