Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amepokea
kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za kuuawa kwa askari 14 wa Jeshi la
Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliopo katika operesheni ya ulinzi wa
amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Pamoja na askari hao
kuuawa, askari wengine 44 wamejeruhiwa na 2 hawajulikani walipo.
Kufuatia vifo hivyo
Mhe. Dkt. Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Waziri wa Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jen. Venance
Salvatory Mabeyo, Maafisa na Askari wa wote JWTZ, familia za marehemu na
Watanzania wote kwa kuwapoteza mashujaa waliokuwa wakitekeleza wajibu wao.
“Nimeshtushwa na
kusikitishwa sana na vifo vya vijana wetu, askari shupavu na mashujaa
waliopoteza maisha wakiwa katika majukumu ya kulinda amani kwa majirani zetu
DRC” amesema Mhe. Dkt. Magufuli.
Amewaombea marehemu
wote wapumzishwe mahali pema peponi, Amina.
Aidha, Mhe. Rais
Magufuli amewataka Watanzania wote kuwa watulivu na kuwa na subira wakati
Serikali ikiendelea kuchukua hatua zinazostahili baada ya kutokea tukio hilo,
na pia amewaombea majeruhi wote wapone haraka ili waweze kuendelea na majukumu
yao ya kawaida.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa
Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chamwino, Dodoma
08 Desemba, 2017
Askari wa 14 wa JWTZ wauawa katika shambulio nchini DR Congo
Reviewed by KUSAGANEWS
on
December 08, 2017
Rating:

No comments:
Post a Comment