Serikali yatenga Bil 22 kwa mwezi



Serikali imesema hivi sasa inatoa sh. bilioni 22.2 kila mwezi ili kuboresha elimu ya msingi na sekondari hapa nchini kuajiri walimu wengi zaidi wa masomo ya sayansi.


Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Bw. George Simbachawene wakati akizungumza na wahitimu 166 wa darasa la saba wa shule ya msingi ya Martin Luther, kwenye sherehe za mahafali ya 10 zilizofanyika shuleni hapo katika Manispaa ya Dodoma.

"Wazazi wa wanafunzi wanaohitimu tunawakaribisha kwenye shule za sekondari kwa sababu zote zina walimu wa kutosha, madawati na vifaa vya kufundishia. Kila mwezi tunatenga sh. bilioni 22.2 kuendesha shule za msingi na za sekondari hadi kidato cha nne," alisema.

Alisema hivi sasa, baadhi ya shule zinakabiliwa na changamoto ndogo ya upungufu wa walimu wa sayansi lakini nayo itatuliwa hivi karibuni kwa sababu vibali vya ajira vimeanza kutolewa.

"Tunaendelea kuziboresha na tumeshuhudia miaka ya karibuni wanafunzi bora kitaifa wakitoka katika shule za Serikali ambazo wengi wamezoea kuziita ni shule za kata. Hakuna shule za kata. Zote ni zimejengwa na Serikali. Ukienda vyuo vikuu wanafunzi wa ufaulu wa juu wengi wao ni wale waliotoka kwenye shule za Serikali," aliongeza.

Pamoja na hayo Simbachawene aliwataka wanafunzi wanaojiandaa kufanya mitihani yao Septemba 6 na 7, wasiwe na hofu kwani kufanya hivyo ni chanzo cha kuwafanya wachanganye mambo na kisha kufeli.
Serikali yatenga Bil 22 kwa mwezi  Serikali yatenga Bil 22 kwa mwezi Reviewed by KUSAGANEWS on September 03, 2017 Rating: 5

No comments: