UHURU KWA BINADAMU

BINADAMU ni kiumbe aliyezaliwa na haki ya uhuru, tena uhuru kamili.

Licha ya kuwa hilo twalifahamu wazi, uhuru wa binadamu huandamana na masharti mengi.

Hii ni kwa kuwa uhuru wa mtu mmoja huweza kuwa na athari kwa mtu mwingine.

Hivyo basi binadamu hufungwa na masharti na sheria chungu nzima za kumdhibiti licha ya kuwa binadamu wamezaliwa huru.

Kunayo mataifa yenye kutawaliwa na madikteta wasiotaka kuskia neno ‘uhuru’ wala ‘haki’.

Na nchi zisizo na madikteta, zimejaa sheria nyingi kupindukia, zote hizo kuhakikisha kuwa kuna amani miongoni mwa waja.

Mbona tudai kuwa watu wana haki ya kuwa huru ila hatuioni haki hiyo ikitekelezeka kokote katika dunia hii ya Mungu?

Au pengine uhuru huo huenda ukawa ni wa kimawazo tu?

Au jawabu bora zaidi ni kwamba uhuru wa mwanadamu ni mawazo yake mwenyewe?

Kwamba sisi wanadamu tuko huru kufikiri lolote tutakalo, kwenda kokote bila kizuizi ila katika mawazo tu!

Ukweli ni kuwa, watu wote wako huru mawazoni kufikiri chochote ila kutenda, tunazuiliwa na vikwazo vya kila aina.

Nadhani uhuru wa kimawazo unasababishwa na uwezo maalum waliokabidhiwa watu na Muumba wao.

Zaidi ya hayo ni kuwa mawazo ni jambo la siri hivyo hayawezi kumwathiri mwingine kwa vyovyote vile.

Katika mawazo yetu, tunao uhuru hata wa kuwaza anachowaza mwingine sasa, alichowaza jana na atakachowaza baadaye!

Tunaweza kutenda jambo lolote mawazoni! Bila kizuizi.

Ila tunaonywa sana kuwa kile tuwazacho wakati mwingine huweza kujitokeza wazi kikawa dhahiri kwa wote!

Hoja hiyo ndiyo pengine huweza kutawala mawazo ya watu lau sivyo, bila shaka tuko huru kabisa kimawazo.

Kutamani kwenda nyumbani

Hebu fikiria hali ya wanafunzi katika shule za mabweni, wanaotamani kwenda nyumbani.

Wao bila shaka huwa mbali kimawazo ila tu miili yao ndiyo huwa shuleni.

Hali hii wakati mwingine huchangia matokeo mabaya katika mtihani wao.

Ila, ni vigumu kwa mtu kutawala mawazo ya mwingine bila hiari yake!

Angaa mawazo yetu hutupa uhuru tunaouthamini kama binadamu.

UHURU KWA BINADAMU UHURU KWA BINADAMU Reviewed by KUSAGANEWS on August 20, 2017 Rating: 5

No comments: